• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Vyuo vitafute karo zaidi kwingineko

TAHARIRI: Vyuo vitafute karo zaidi kwingineko

KITENGO CHA UHARIRI

MZOZO ambao umeibuka kufuatia pendekezo la kuongeza karo ya wanafunzi, unarudisha nyuma hatua zilizopigwa katika kuboresha kiwango cha elimu ya juu nchini.

Utata huo unafuatia pendekezo lililowasilishwa na wakuu wa vyuo hivyo kwa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, mnamo Jumatano wakitaka karo ya chio iongezwa kutoka Sh16,000 hadi Sh48,000 kwa kila mwanafunzi.

Ingawa pendekezo hilo bado halijaidhinishwa, kwani linatarajiwa kuwasilishwa kwa Baraza la Mawaziri hapo Januari, limekosolewa vikali na wanafunzi pamoja na wadau wengine wakilalamika kutofahamishwa wala kushirikishwa.

Ni malalamishi yaliyomfanya Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, kujitokeza jana na kuwarai wanafunzi kuwa watulivu.

Vile vile, Waziri Magoha alikosoa pendekezo hilo akisema ni makosa kwa wakuu wa vyuo kuongeza karo karibu mara tatu zaidi, bila kuwashirikisha wadau wote.

Ingawa wasimamizi hao wanataja uhaba wa fedha vyuoni kama chanzo kikuu cha hatua hiyo, ingekuwa vizuri ikiwa mchakato huo ungeendeshwa kwa kuhusisha maoni ya wadau wote husika.

Ni dhahiri kwamba vyuo vikuu nchini vimekuwa vikipitia hali ngumu kifedha, huku baadhi vikiwafuta kazi mamia ya wafanyakazi wake, hasa tangu janga la virusi vya corona kutua nchini mnamo Machi.

Vingine vimelazimika kufunga baadhi ya matawi yake kutokana na upungufu mkubwa wa wanafunzi. Sababu nyingine ya masaibu hayo ni kupungua kwa kiwango cha fedha ambazo vinapokea kama ufadhili kutoka kwa Serikali, ili kuendesha shughuli zake.

Bila shaka, taswira hiyo imewaacha wasimamizi hao kwenye njiapanda, wakijikuna vichwa kuwazia hatua watakazochukua kuhakikisha taasisi hizo muhimu zinajisimamia kifedha ili kuepuka hatari ya kufilisika.

Hata hivyo, ikizingatiwa si vyuo vikuu pekee vimejikuta katika hali hiyo, wakuu wanapaswa kubuni njia mbadala za kupata fedha, badala ya kuwabebesha wanafunzi mzigo wasiostahili.

Ugumu ambao vyuo vinapitia unapaswa kuvifungua macho ili vibuni mbinu shupavu za kujipatia fedha, kwa mfano kupitia uwekezaji wa teknolojia.

Ndivyo vyuo vingine duniani vinafanya kama njia ya kuhimili athari za janga la corona. Isitoshe, kwa kufanya hivyo huenda hiyo ikawa hatua ya kwanza katika kutatua baadhi ya matatizo yanayoviandama.

You can share this post!

Hatua ya UN ‘kuhalalisha’ bangi yasifiwa na...

Viongozi wawahimiza wakazi wa Thika wakubali BBI, baadhi...