• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Nyanya ziko sokoni kwa wingi

Nyanya ziko sokoni kwa wingi

Na SAMMY WAWERU

KUFUATIA dadi kubwa ya watu walioathirika kutokana na mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini mnamo Machi 2020, wengi waliingilia shughuli za kilimo.

Mamia ya maelfu walipoteza nafasi za ajira, huku baadhi ya biashara zikifunga milango yake kwa kushindwa kustahimili makali na athari za virusi vya corona.

Utafiti unaonyesha wengi walirejea mashambani ili kusukuma gurudumu la maisha. Wenye ploti mijini na kwa bahati nzuri wana vipande vya ardhi mashambani, wamezigeuza kitega uchumi.

Emmah Wanjiru ambaye ni mtaalamu wa kilimo, nyanjani katika kampuni ya H.M Clause, anasema akilinganisha kiwango cha wateja anaohudumia mwaka huu, 2020 na miaka ya awali, kuna tofauti kubwa.

“Idadi ya wateja 2020 imeongezeka mara dufu, kutokana na takwimu za mauzo ya mbegu ya mazao yanayochukua muda mfupi kukomaa tunazounda,” Wanjiru anaelezea.

Kulingana na mtaalamu huyo, mambo ni bayana kule nyanjani kutokana na ongezeko la wakulima.

Mkulima akionyesha mazao ya nyanya. Kipindi hiki cha corona kumekuwa na ongezeko la zao la nyanya nchini. Picha/ Sammy Waweru

Akitumia mfano wa nyanya, Wanjiru amesema idadi ya wakulima wanaokuza zao hilo ni ya juu.

“Ukitembea kwenye masoko mbalimbali nchini, utagundua mazao ya nyanya ni tele. Wengi wa walioathirika na corona wamekumbatia kilimo kujiendeleza kimaisha,” akasema.

Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo katika masoko kadha viungani mwa jiji la Nairobi, kiwango cha nyanya ni cha juu, huku kundi la nyanya 4 au 5 likiuzwa Sh10.

“Mazao mengine tunalazimika kuyauza nyanya moja Sh1,” akasema Mama Njambi ambaye ni mchuuzi wa mazao mbichi ya kilimo Githurai.

Nicholas Mwangi ni mkulima wa nyanya na vitunguu eneo la Mai Mahiu, na ambaye aliingilia shughuli za kilimo baada ya kazi yake kuathirika na virusi vya corona.

“Nilikuwa katika sekta ya utalii, na ambayo imeathirika pakubwa. Sikuwa na budi ila kuingilia kilimo, nyanya na vitunguu vikiwa chaguo la kwanza,” Nicholas anadokeza.

Licha ya kuwepo kwa nyanya nyingi nchini, zinazokosa kununuliwa zinaishia kuharibika. Wakulima na wafanyabiashara wanahimizwa kukumbatia mfumo wa kuongeza mazao thamani, kama vile kuunda sosi zinazotokana na nyanya.

  • Tags

You can share this post!

Neymar atamani tena kucheza pamoja na Messi

Mourinho atilia shaka uzalendo wa baadhi ya wanasoka wake...