Michezo

Wanaraga wa Kenya Simbas wapata mwaliko wa kucheza dhidi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas, imepangiwa kushiriki mechi mbili dhidi ya kikosi mseto cha Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini mnamo Aprili 2021.

Kocha Paul Odera amesema kwamba ni vyema kwa kikosi hicho kusalia katika hali ya ushindani baada ya kampeni za msimu mzima wa 2020 kufutiliwa mbali kutokana na janga la corona.

Ili kufanikisha kampeni za Kenya Simbas dhidi ya Stellenbosch, kikosi hicho kimewaajiri wakufunzi wawili raia wa Afrika Kusini – Neil De Kock ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok’ na Ernst Joubert ambaye ni nahodha wa zamani wa kikosi cha Saracens.

Huku De Kock akitarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi, maarifa ya Joubert yatategemewa sana katika juhudi za kuboresha makali ya idara ya mbele.

Wakufunzi hao wawili walitarajiwa pia kukinoa kikosi cha wanaraga chipukizi wa Kenya U-20 almaarufu ‘Chipu’ kwa minajili ya kampeni za kipute cha Barthes Cup kilichoahirishwa pia mwaka huu kwa sababu ya corona.

Ni matumaini ya Odera kwamba Wizara ya Michezo itawapa wanaraga wa Simbas idhini ya kuanza maandalizi mnamo Januari 2021 ili kujifua vilivyo kwa kipute dhidi ya Stellenbosch.

“Tunatarajia pia kupata idhini ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kuanza mazoezi kwa minajili ya michuano hiyo ijayo nchini Afrika Kusini. Iwapo wachezaji watashiriki mazoezi kwa kipindi cha miezi mitatu au minne kwa kuzingatia kanuni zote zilizopo za kudhibiti maambukizi ya Covid-19, basi tutajiweka pazuri zaidi kutamba nchini Afrika Kusini,” akasema Odera.

Shujaa na Lionesses tayari wamepewa idhini ya kuanza kujiandaa kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.

“Kwa kuwa sasa hakuna mechi za ligi na wanaraga wengi hawajashiriki michezo yoyote kwa takriban miezi minane iliyopita, tutategemea zaidi wachezaji waliotuwajibikia mwaka uliopita wa 2019. Hao ndio tutakaowaita kambini baada ya kupata idhini ya Serikali kupitia KRU,” akaeleza Odera.

Odera ambaye pia amewahi kuchezea timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, amesema mustakabali wa kampeni za Kombe la Afrika almaarufu Africa Cup utajulikana mwishoni mwa wiki ijayo baada ya makocha wa mataifa wanachama kushiriki mkutano wa mtandaoni na vinara wa Shirikisho la Raga la Afrika (Rugby Africa).

Ili kufanikisha ziara yao ya kutua Afrika Kusini, Odera amesema kwamba kikosi cha Kenya Simbas kitahitaji takriban Sh20 milioni na mipango ya kuchangia kikosi hicho kwa minajili ya mechi za siku 11 nchini Afrika Kusini tayari imeanza.

Odera pia ameshikilia kwamba italazimu vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu ya Kenya Cup kuimarisha viwango vyao vya mchezo ili kuwezesha timu ya taifa ya Shujaa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

“Kuboreka kwa kikosi cha taifa na kusalia hai kwa matumaini ya timu hiyo kufuzu kwa Kombe la Dunia kutategemea kuimarika kwa raga yetu katika viwango vya ligi. Nimekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na baadhi ya wakufunzi wa vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu na tumeshauriana kuhusu jinsi ya kuimarisha ushindani katika idara mbalimbali za vikosi vyao,” akasema Odera.