Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa mawasiliano na dhima yake katika kujifunza lugha ya Kiswahili

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KUFAHAMU kuhusu umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili husaidia kuelewa matatizo yanayowakumba wakufunzi na wanafunzi wa lugha katika mchakato wa ujifunzaji lugha na pia jinsi ya kusuluhisha matatizo hayo.

Kwa mujibu wa Canale na Swain (1980) umilisi wa lugha hutekeleza majukumu anuai huku mtaalam Stern (1983) akiunga mkono kauli hiyo kwa kuhoji kwamba lugha ni jukumu mojawapo ambalo halina budi kutekelezwa.

Msemaji wa lugha hiyo sharti awe na umilisi wa kuweza kutumia lugha vilivyo na awe mwepesi wa kuunda maneno na sentensi.

Carol (1968) anahoji kwamba umilisi wowote wa lugha huhusisha umilisi wa kiisimu na kiutendaji katika lugha husika ambapo mtu huwa na ujuzi wa kuzungumza lugha yoyote ile ikiwa ana umilisi wa matumizi ya lugha.

Msomi Clark (1977) anaafikiana na hoja hiyo ambapo anafafanua kuwa mtu aliye na weledi katika lugha ni sharti awe na ufahamu na uelewa wa kanuni anuai ikiwemo kileksia, kifonolojia, kisintaksia, kisemantiki na uchanganuzi usemi katika muktadha wa kijamii.

Kwa upande wao Habwe na Karanja (2004) wanahoji kuwa lugha ni mali ya jamii na huhusiana na mambo ya kijamii.

Umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili hivyo basi hutegemea mambo mbalimbali kama vile mazingira anamokulia mtu ambapo mtu akiwa katika mazingira yenye umilisi mkubwa wa kiisimu basi weledi wake huweza kuongezeka na kufikia upeo wa juu wa asilimia sabini na tano au zaidi.

Wasomi wengine tajika ambao wamebobea katika ufafanuzi wa dhana kuhusu umilisi wa lugha ni pamoja na Hymes (1971), Canale na Swain (1980), Nicuolo (1991), Nunan (2003) pamoja na Flutcher na Davidson (2007).

Mwasisi wa nadharia ya umilisi wa lugha ni mwanaisimu maarufu Noam Chomsky (1965) ambaye anafafanua umilisi wa lugha kama ule uwezo wa mzungumzaji wa kufahamu vyema kanuni za kiisimu na sheria lugha anayoizungumza.

Sheria hizo ni pamoja na leksia, fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki jinsi tulivyotaja hapo awali.

Kando na kufahamu kanuni za lugha, mtaalam huyu anahoji kwamba ni sharti mwanafunzi wa lugha awe na uwezo wa kutumia lugha jinsi ipasavyo.

[email protected]

Marejeo

Gardner, R.C. (1985). Social Psychology and Second Language Learning: The Role of Attitude and Motivation. London: Edward Arnold.

Gardner, R. & Smythe, P. C. (1981). On the development of the Attitude/Motivation Test Battery. Canadian Modern Language Review.