• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa usemaji kama kitengo cha uamilifu katika lugha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa usemaji kama kitengo cha uamilifu katika lugha

Na MARY WANGARI

MSOMI Chomsky ambaye ni mwasisi wa nadharia ya umilisi wa kiisimu katika lugha anahoji kwamba ni sharti mwanafunzi wa lugha awe na uwezo wa kutumia lugha ipasavyo kando na kufahamu kanuni za lugha husika.

Hata hivyo, mwanaisimu Hymes (1971) anataja mtazamo wa Chomsky kuhusu umilisi wa lugha kama ulio finyu akihoji kwamba unaegemea tu katika masuala ya kiisimu.

Anafafanua kwamba kuzifahamu sheria za kiisimu za lugha pekee hakutoshi kumwezesha mtu kuweza kuitumia lugha kikamilifu katika jamii yake.

Ni kwa mintarafu hiyo ambapo Hymes na wataalam wengine wa lugha ikiwemo Savignon (1972) walipambanua mawazo ya Chomsky kuhusu umilisi wa lugha kwa kuanzisha dhana ya umilisi wa mawasiliano.

Kando na kuhusisha umilisi wa sheria za lugha, Hymes anahoji kwamba umilisi wa mawasiliano pia huhusisha masuala ya kiisimujamii ya lugha kama vile utendaji wa lugha ama ule uwezo wa kutumia lugha kwa ufaafu katika miktadha mbalimbali ya kijamii.

Mitazamo ya wataalam hao wa lugha inasaidia mwanafunzi na mwalimu kuelewa matapo mbalimbali kuhusu umilisi wa kiisimu katika lugha.

Aidha, uelewa huu husaidia kuchunguza dhana ya ulimisi wa kiisimu pamoja na umilisi wa mawasiliano kama kitengo cha utendaji.

Umilisi wa usemaji – Mwanaisimu Newmark (1966) anadai kwamba ni sharti mtu afahamu mambo kadhaa kama vile sheria za kimsingi za lugha, umilisi wa usemaji, umilisi wa isimujamii na kadhalika ili asheheni umilisi wa kiwango cha wastani au cha upeo wa juu zaidi.

Mtazamo wake unaungwa mkono na Richard na Rodgers (1986) wanaodai kwamba si rahisi kwa mtu kusema ana umilisi wa lugha kwa sababu umilisi wa lugha unahusu mambo mengi sio tu umilisi wa kanuni za lugha na utendaji.

Mfano mzuri ni sentensi za Kiswahili zinazohusisha kiima na kiarifa kuhusiana na sheria ambazo zimekubaliwa na wanajamii lugha husika. Kwa mfano:

Rais anatoa hotuba.

Watahiniwa wanafanya mtihani.

Katika sentensi hizi, ‘Rais’ ni kiima na ‘anatoa hotuba’ ni kiarifa.

Watahiniwa ni kiima na ‘wanafanya mtihani’ ni kiarifa.

Mtindo huu hufuatwa katika sentensi zote katika lugha ya Kiswahili. Ni makosa kisarufi kwa sentensi kuanza na kiarifa kisha ifuatwe na kiima kwa sababu hazitakuwa na mantiki na maana iliyokusudiwa na mwandishi itapotoshwa.

Hivyo basi, ni vyema kuelewa kuwa mpangilio wa sentensi ya Kiswahili hufuata muundo maalum ambao ukibadilishwa sentensi huwa na maana tofauti na ilivyokusudiwa.

[email protected]

Marejeo

Gardner, R. & Smythe, P. C. (1981). On the development of the Attitude/Motivation Test Battery. Canadian Modern Language Review.

Tewes, U. (1991). Intergration of visual and linguistic information in spoken language. Toronto: Wechesler pub.?

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa mawasiliano na dhima...

Acha katambe