TAHARIRI: Klabu zetu zijiimarishe barani
KITENGO CHA UHARIRI
TANGU Gor Mahia iwaletee Wakenya fahari ya kihistoria iliposhinda Kombe la Afrika kati ya klabu mnamo 1987, hapajawahi kutokea tena kuwa timu ya nchi hii imepiga hatua ya maana katika soka ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Katika miaka hiyo ya ’70 na ’80 timu za Kenya ziliogofya sana barani ikiwemo timu ya taifa Harambee Stars.
Japo Stars haikuwahi kushinda kombe lolote Afrika au hata kupiga hatua ya maana, wapinzani waliiogopa sana hasa tunaporejelea kandanda ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Klabu kongwe za humu nchini zikiwemo AFC Leopards, Gor Mahia, Bandari, Tusker na Ulinzi pamoja na nyinginezo mpya mathalani Sofapaka zimekuwa zikifuzu kwa mashindano mbalimbali ya CAF lakini aghalabu huwa zinaondolewa katika hatua za mwanzo kabisa.
Gor na Sofapaka ziliwahi kujaribu kupiga hatua ya maana mara si nyingi lakini bado hazikuweza kuvuka hatua inayoweza kuvutia umakinifu wa mashabiki na wapenzi wa mchezo huu barani.
Sharti tuchunguze ni kitu gani kinachofanya Kenya kubaki nyuma kiasi hiki katika wanda la mchezo huu licha ya kwamba mataifa tulioanza kushindana nayo katika kandanda miaka ya ‘60 kama vile Ghana na Nigeria yamepiga hatua ya kujivunia.
Inakuwaje kwamba timu yetu ya taifa haijawahi kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia hata mara moja?
Kwa jicho la ndani, vipo vizingiti vinavyosababisha taifa letu kusalia mkiani kwenye fani ya kandanda. Zipo siasa chafu katika uongozi wa kandanda nchini kuanzia kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).
Pia kuna ufadhili mdogo mbali na kukosa mfumo mzuri wa kuteua wanasoka stadi wanaoweza kupambana na majabari wa soka barani na duniani. Imewahi kutajwa kuwa klabu za Kenya huamua ‘kuuza’ mechi ili kuepuka gharama nyingi zinazoandamana na mechi za bara. Hii ni ishara tosha kuwa klabu zetu hazijawezesha kifedha kumudu mechi za haiba ya barani.
Majuzi kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi pamoja na benchi lake la ufundi walifutwa bila sababu yoyote inayojulikana.
Ripoti nyingi zilisema kuwa hatua ya kumfuta kocha huyo ilitokana na siasa za kandanda. Iwapo hilo ni kweli, basi Kenya itasalia kwenye giza kwa muda mrefu hadi tutakapozinduka.
Wakenya twahitaji hatua ya maana katika soka. Sharti kinara wa FKF, Nick Mwendwa atueleze anafanya nini ili kuhakikisha tunajionea fahari katika mchezo huu unaopendwa zaidi duniani.
Tangu Gor Mahia iwaletee Wakenya fahari ya kihistoria iliposhinda Kombe la Afrika kati ya klabu mnamo 1987, hapajawahi kutokea tena kuwa timu ya nchi hii imepiga hatua ya maana katika soka ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).