• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Mbappe afikisha mabao 100 akivalia jezi za PSG

Mbappe afikisha mabao 100 akivalia jezi za PSG

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe alifunga bao lake la 100 akivalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) na kusaidia viongozi hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kuwapepeta Montpellier 3-1 mnamo Disemba 5, 2020.

Colin Dagba aliwaweka PSG kifua mbele katika dakika ya 33 kabla ya Stephy Mavididi, 22, kusawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Goli la Dagba ambalo lilikuwa lake la kwanza kambini mwa PSG, lilichangiwa na fowadi Angel Di Maria.

Sajili mpya wa PSG, Moise Kean alipachika wavuni bao la pili la PSG katika dakika ya 77 kabla ya Mbappe kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mbappe, 21, alifunga bao hilo la 100 akiwa mchezaji wa PSG baada ya kuwajibishwa katika jumla ya michuano 137 na miamba hao wa soka ya Ufaransa.

Anakuwa sasa mchezaji wa tano kuwahi kufikia idadi hiyo ya mabao akivalia jezi za PSG. Wengine waliowahi kumtangulia ni Edinson Cavani (200), Zlatan Ibrahimovic (156), Pauleta (109) na Dominique Rocheteau (100).

“Nimekuwa nikitamani fursa ya kufunga mabao katika takriban kila mchuano, lakini si kufikia rekodi hii ninayojivunia kwa sasa. Nilipojiunga rasmi na kikosi hiki cha PSG, sikuwahi kuwazia kabisa kuhusu uwezekano wa kufunga hata mabao matatu. Lakini sasa nina 100 kutokana na mechi 137 pekee,” akasema Mbappe akiwa mwingi wa shukran kwa wachezaji wenzake na benchi ya kiufundi ya PSG.

Nyota huyo raia wa Ufaransa alifunga pia jumla ya mabao 27 akiwa mchezaji wa AS Monaco kabla ya kutua PSG kwa kima cha Sh23 bilioni.

Fowadi matata wa PSG, Neymar Jr ambaye ni raia wa Brazil alipumzishwa katika mechi hiyo dhidi ya Montpellier huku Mbappe akiingia uwanjani katika kipindi cha pili.

Kiini cha hatua hiyo ya kocha Thomas Tuchel ni kukiandaa kikosi chake vilivyo kwa mchuano wa kufa-kupona utakaowakutanisha PSG na Istanbul Basaksehir mnamo Disemba 8, 2020 ugani Parc des Princes, Ufaransa.

You can share this post!

Wakazi Lamu waandamana kupinga ongezeko la visa vya unajisi...

Real Madrid washinda kwa mara ya kwanza baada ya michuano...