• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Wakazi wa jiji wajiandaa kufurika vijijini kwa Krismasi

Wakazi wa jiji wajiandaa kufurika vijijini kwa Krismasi

Na WAANDISHI WETU

LICHA ya Wakenya wengi kulalamikia makali ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la corona, wakazi wengi Nairobi wanapanga kusafiri maeneo ya mashambani kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Pitapita za Taifa Leo katika vituo vya mabasi ya abiria ya masafa marefu jijini Nairobi jana zilibaini kuwa tayari yamejaa hadi Desemba 26.

Hii ni licha ya kwamba nauli tayari zimepandishwa kwa zaidi ya asilimia 50 juu ya kiwango kilichopandishwa wakati wa janga la corona.

“Kufikia leo (Jumapili) asubuhi viti vyote katika mabasi yetu ya kuelekea ruti zote za magharibi mwa Kenya vilikuwa vimelipiwa hadi Desemba 26. Nafasi zilizoko ni za kuanzia Desemba 27 na tunabashiri kuwa kufikia wiki kesho vitakuwa vimejaa,” akasema mhudumu mmoja wa kampuni ya Guardian Angel, jina lake linabanwa.

Katika kampuni ya Modern Coast nafasi katika mabasi ya kuelekea magharibi mwa Kenya tayari zimejaa hadi Desemba 25.

Hata hivyo katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu walisema bado watu hawajapanga kusafiri kwa wingi.

“Biashara si nzuri sana, tunahisi watu bado wanahofia kusafiri kutokana na virusi vya corona,” akasema Bw Lennox Shallo, Meneja wa mabasi ya Mash.

Bw Ajaz Mirza wa kampuni ya Coast Bus alisema wana matumaini biashara itaimarika sikukuu ya Krismasi itakapokaribia.

Wakati huo huo, wawekezaji katika sekta ya utalii wamewaonya magavana dhidi ya kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuweka sheria ya kuzuia watu kusafiri kutoka maeneo yao kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mwenyekiti wa wawekezaji wa utalii nchini Bw Mohammed Hersi, alisema hatua hiyo ya magavana ni hatari kwa uchumi wa taifa. Haya yanajiri siku chache baada ya wamiliki wa mahoteli ya kifahari eneo la Pwani kuisihi serikali kutofunga nchi wakisema utalii umeathirika pakubwa na janga la corona.

Kulingana na takwimu kutoka shirika la utafiti wa utalii nchini, Kenya ilipokea wageni 470,971 kati ya Januari hadi Oktoba 2020 ikilinganishwa na wageni 1.7 milioni wa kimataifa mwaka 2019.

Ripoti za Charles Wasonga, Mishi Gongo na Winnie Atieno

You can share this post!

Tottenham wafunga mawili na kuendeleza ubabe wao dhidi ya...

COVID-19: Kenya yafikisha visa jumla 88,380 idadi ya vifo...