• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Nzige: Onyo Wapwani wasiwafanye kitoweo

Nzige: Onyo Wapwani wasiwafanye kitoweo

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Kaunti ya Kilifi wameonywa dhidi ya kula nzige ambao wameshambulia eneo hilo.

Onyo hilo limetolewa na serikali ya Kaunti baada ya kubainika kuna wakazi wamegeuza nzige kitoweo licha ya kuwa wamenyunyiziwa dawa yenye sumu.

Maeneo ambayo nzige wameathiri kwa wingi ni Magarini, ambapo zaidi ya ekari 950 za mimea tayari zimeharibiwa na wadudu hao huko Marafa na Garashi.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi alisema maafisa wa kilimo tayari wametumwa kwenye kaunti ndogo ya Magarini ambako wadudu hao walionekana kwa mara ya kwanza ili kukabiliana na kumaliza tatizo hilo.

Bw Kingi pia aliwaonya wakazi dhidi ya kuwafurusha nzige wanaotua misituni na vichakani, akisisitiza kuwa hali hiyo huenda ikaleta athari zaidi za mashamba kuvamiwa na nzige eneo hilo.

“Tunafanya juhudi kukabiliana na hawa nzige na kuwamaliza eneo hili. Kuna maafisa wa kilimo ambao wamekuwa mashinani. Tunafanya mipango kuwaangamiza wadudu hao ili kusiwe na athari mbaya zaidi kwa mimea yetu,” akasema Bw Kingi.

Serikali kuu kwa ushirikiano na serikali za kaunti imezidisha harakati zake za kukabiliana na kuwamaliza nzige wanaovamia kaunti mbalimbali za Ukanda wa Pwani.

Yamkini ekari zaidi ya 1,500 za mimea tayari zimeripotiwa kuathiriwa na wadudu hao katika kaunti za Lamu, Kilifi, Tana River na Taita Taveta.

Katika kaunti ya Lamu, ekari takriban 500 zimeripotiwa kuharibiwa na wadudu hao katika maeneo mengi.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alisema wataalamu wametumwa kutoka Nairobi ili kutekeleza usoroveya na kunyunyizia kemikali wadudu hao katika maeneo yote yaliyovamiwa.

“Usoroveya wa angani na nchi kavu unaendelea ili kutathmini maeneo halisi ambayo nzige hao wamekita kambi. Timu iko hapa na inashirikiana na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Lamu ili kuanza kunyunyiza dawa za kuua nzige kuanzia juma hili,” akasema Bw Macharia.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, serikali kuu pia imekuwa ikiendeleza juhudi za kuwaangamiza nzige eneo hilo.

Waziri wa Kilimo wa Taita Taveta, Bw Davis Mwangoma alisema uvamizi wa nzige eneo hilo umekabiliwa vilivyo kwani shughuli za kunyunyizia dawa na kuua wadudu hao na mayai yao zimekuwa zikiendelea tangu juma lililopita.

Kulingana na Bw Mwangoma, maafisa kutoka kitengo cha kukabiliana na wadudu nchini wamekuwa wakipuliza dawa na kuua nzige ambao walikuwa wamevamia mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Tsavo iliyoko Voi.

Afisa huyo aidha alisema sehemu ambazo hazijanyunyiziwa dawa ya kuua nzige ni Ngolia, Mwatate na kaunti ndogo ya Taveta.

“Shughuli ya kupuliza dawa na kuua nzige imetekelezwa kwenye mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Tsavo Magharibi na maafisa husika wa serikali kuu kwa ushirikiano na kaunti bado wanakadiria hali kuona iwapo nzige hao pia watasambaa sehemu zingine ili wakabiliwe zaidi,” akasema Bw Mwangoma.

Ripoti za Kalume Kazungu, Maureen Ongala na Lucy Mkanyika

You can share this post!

Pondeni raha mkijua Januari ni shule – Magoha

Seneti kuamua jinsi Sonko atakavyojitetea