Makala

TAHARIRI: Tutajuta kupuuza masuala ya dharura

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KITENGO CHA UHARIRI

INASIKITISHA jinsi siasa zinazidi kuteka mawazo ya wananchi wengi wakati huu ambapo taifa linakumbwa na majanga chungu nzima.

Janga la corona lilileta matatizo mengi kwa taifa hili, hasa katika sekta ya uchumi, elimu, afya miongoni mwa nyingine.

Hatukatai kuwa maisha yafaa kuendelea mbele, ikiwemo masuala ya kisiasa, lakini mambo ambayo si ya dharura yanafaa yaekwe kando kwa sasa.

Badala yake tutumie nguvu na rasilimali zilizopo kulinda afya na maisha ya umma.

Wahudumu wote wa afya wametishia kuanza mgomo leo kitaifa ilhali midahalo inayoendelezwa na wanasiasa ni kuhusu masuala ambayo si ya dharura.

Tangu wakati Kenya ilipoanza kuwa na uongozi wa ugatuzi mwaka wa 2013, sekta ya afya imepitia changamoto tele sawa na mafanikio ambayo yameonekana sehemu nyingine za nchi.

Kuna serikali za kaunti ambazo kwa kweli zimejikakamua kuimarisha utoaji huduma za afya katika hospitali za umma.

Kaunti hizo ndizo zimefanya ionekane kuwa ilikuwa hatua nzuri kuweka usimamizi wa afya, hasa uboreshaji miundomsingi, chini ya mamlaka ya serikali za kaunti.

Hata hivyo, kungali kuna kaunti nyingine nyingi ambazo hazijali kamwe kuhusu umuhimu wa kutoa huduma bora za afya kwa umma.

Ni kaunti hizi ambazo hufanya baadhi yetu kujuta kwa nini taifa likaruhusu jukumu la afya kuwa chini ya magavana.

Katika kaunti hizo, utasikia wagonjwa na madaktari wakieleza wasiwasi wao kila mara wanapoingia hospitalini kwani wote wanaweka maisha yao hatarini.

Vile vile, serikali kuu hulaumiwa kwa kuchelewa kutuma pesa kwa kaunti na hivyo kuchelewesha mishahara ya wahudumu.

Haya ni masuala ambayo yangehitajika kupewa kipaumbele na taifa zima ili kupatikane suluhisho la kudumu kuhusu malalamishi ya mara kwa mara kutoka kwa wahudumu wa afya.

Katika uchumi, taifa lingali linabeba mzigo mzito wa madeni, huku mapato ya kitaifa yakipungua sana mwaka huu.

Haya yanaendelea wakati ambapo watoto wote watahitajika kurudi shuleni Januari, ilhali hatuoni kama kuna dalili zozote za hatua mwafaka kuchukuliwa mapema kuboresha miundomsingi shuleni ili iambatane na kanuni za kuepusha maambukizi ya janga la corona.