VIKEMBE: Diogo Jota, nguli wa kukamilisha mavamizi
Na GEOFFREY ANENE
DIOGO Jose Teixeira da Silva almaarufu Diogo Jota ni mmoja wa wachezaji wanaovuma uwanjani Anfield na Uingereza kwa jumla wakati huu.
Winga huyo alizaliwa mjini Porto nchini Ureno Desemba 4, 1996. Diogo ni mkali katika kukamilisha mashambulizi.
Mapenzi ya wazazi wake Joaquim na Isabel Silva katika soka yalishuhudia Diogo akiungwa mkono alipoanza uchezaji wake katika klabu ndogo ya Gondomar nchini mwake akiwa na umri wa miaka tisa. Haikumchukua muda mrefu kazi yake ya kuridhisha kuonekana akiingia katika timu za wachezaji waliomzidi umri kwa haraka.
Alinyakuliwa na Pacos de Ferreira mwaka 2013. Pacos inasifika sana kwa kukuza talanta changa nchini Ureno. Hakutumia fursa hiyo vibaya. Aliichukua kwa mikono miwili. Alijiimarisha kimchezo. Alifungia timu ya Pacos ya wachezaji walio chini ya umri wa miaka 17 mabao matano katika mechi mbili zilizopigwa wikendi moja na kusifiwa na kocha Ruben Carvalho aliyetabiri Jota ataenda mbali katika uchezaji wa soka ya malipo.
Mwaka 2014, Jota alijumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Pacos. Alichukulia fursa hiyo kwa uzito. Alianza kuandikisha rekodi za ufungaji wa mabao moja baada ya nyingine. Aliingia katika kumbukumbu za historia za Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuwahi kufungia Pacos. Isitoshe, alipata sifa ya kuwa kikembe aliyefungia klabu yoyote nchini Ureno mabao mawili baada ya mchezaji wa zamani wa Sporting Lisbon, Cristiano Ronaldo.
Msimu 2015-2016 ulishuhudia Diogo akijaza wavuni mabao 14 na kumegea wenzake pasi 10 zilizozalisha magoli katika mashindano yote. Ufanisi huu ulifanya awe mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 12 katika msimu mmoja akiwa na umri wa miaka 19. Aliibuka mchezaji bora mchanga kwenye Primeira Liga msimu huo.
Mchezo wake ulivutia klabu kubwa nchini Ureno. Alizipuuza na kujiunga na Atletico Madrid nchini Uhispania. Hata hivyo, Atletico ilimpeleka Porto kwa mkopo msimu 2016-2017 na Wolverhampton Wanderers 2017-2018.
Alikuwa katika timu ya Porto iliyoaibisha Leicester City 5-0 kwenye Klabu Bingwa Ulaya 2016. Alisukuma kimiani bao la mwisho katika mchuano huo. Alipata bao hilo siku chache tu baada ya kusherehekea kugonga miaka 20 akiingia katika mabuku ya historia kwa kuwa kinda wa kwanza Mreno kupata bao akivalia jezi ya Porto katika mashindano hayo.
Aliondoka Porto msimu uliofuata na kujiunga na Wolves iliyokuwa katika Ligi ya Daraja ya Pili Uingereza. Uhamisho huo uligawanya mashabiki. Wengi hawakuamini macho yao kuwa Jota anagura klabu kubwa nchini Ureno, Porto, kujiunga na Wolves katika daraja ya pili.
Familia yake na mashabiki wachache, hata hivyo, walisimama naye katika hatua aliyochukua chini ya wakala mtajika Jorge Mendes.
Uwanjani Molineux, Diogo aliungana na Ruben Neves waliyecheza pamoja naye Porto, na kocha Mreno Nuno Espirito Santo.
Uamuzi wake ulijitokeza kuwa wa busara kwani aliibuka shujaa katika kampeni safi ya ‘mbwa mwitu’ wa Wolves baada ya kupachika mabao 17 ikiingia Ligi Kuu na kusainiwa kabisa na klabu hiyo kwa msimu 2018-2020.
Alithibitisha yumo mbioni kuwa supastaa alipoingia pia katika historia ya Ligi Kuu ya Uingereza kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Wolves kufunga mabao matatu katika mechi moja. Alipata ‘hat-trick’ hiyo dhidi ya Leicester.
Hata hivyo, ushindani mkali uwanjani Molineux ulishuhudia akichezeshwa kwa uchache katika msimu wake wa mwisho kabla ya Liverpool kumsaini Septemba 2020 kwa kandarasi ya miaka mitano.
Yeye ndiye mshambuliaji ghali katika historia ya ‘The Reds’. Kocha Jurgen Klopp alimnyakua kwa Sh6.7 bilioni. Jota ni mchezaji wa kwanza tangu Robbie Fowler mwaka 1993 kufungia Liverpool mabao saba katika mechi zake 10 za kwanza. Pia, ni mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufunga mabao katika michuano minne ya nyumbani ya Liverpool ligini.
Alipata mafanikio hayo Novemba 22 baada ya kupata bao katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Leicester. Alitawazwa mchezaji bora wa Livepool wa mwezi Oktoba. Diogo amechezea timu ya taifa ya Ureno mara 10. Amefunga mabao dhidi ya Uswidi (mawili) na Croatia (moja) kwenye Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya ya msimu 2020-2021. Analipwa mshahara wa Sh13.4 milioni kila wiki.