Liverpool waponda Wolves na kuwapa mashabiki wao raha uwanjani Anfield
Na MASHIRIKA
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool, waliwakaribisha mashabiki wa soka katika uwanja wao wa Anfield kwa mara ya kwanza tangu Machi 2020 kwa ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Wolves mnamo Disemba 6, 2020.
Mohamed Salah aliwapa Liverpool uongozi katika dakika ya 24 baada ye beki wa Conor Coady wa Wolves kuzidiwa maarifa na nahodha Jordan Henderson.
Georginio Wijnaldum na Joel Matip walifunga bao kila mmoja katika kipindi cha pili kabla ya beki Nelson Semedo kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili.
Wolves walionekana kuzidiwa maarifa katika kila idara kuanzia dakika ya kwanza hadi refa Craig Pawson alipowapa penalti kwa kudhania kwamba Sadio Mane alikuwa amemchezea visivyo Coady ambaye ni difenda wa zamani wa Liverpool. Hata hivyo, maamuzi hayo ya refa yalibatilishwa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha vinginevyo.
Ushindi wa Liverpool uliwadumisha kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama sawa na Tottenham Hotspur waliowazamisha Arsenal 2-0 kwenye gozi la London Kaskazini.
Wolves kwa upande wao walisalia katika nafasi ya 10 kwa alama 17 sawa na Everton, Southampton na West Ham United. Ingawa hivyo, ni pengo la pointi mbili pekee ndilo linalowatenganisha na nambari tano Manchester United ambao kwa pamoja na Manchester City, Southampton, Brighton, Newcastle United na Burnley, wana mechi moja zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na washindani wengine.
Mbali na Salah, Georgio Wijnaldum na Joel Matip, wanasoka wengine waliomtatiza pakubwa kipa Rui Patricio wa Wolves ni Andy Robertson na Roberto Firmino aliyeondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili na nafasi yake kutwaliwa na sajili mpya Diogo Jota.
Beki Trent Alexander-Arnold alirejea katika kikosi cha Liverpool baada ya kupona jeraha na alichangia bao la nne lililofungwa na Semedo baada ya kuzidiwa na presha kutoka kwa Mane.
Wolves walisafiri uwanjani Anfield kwa minajili ya mchuano huo dhidi ya Liverpool bila ya huduma za fowadi matata Raul Jimenez aliyepata jeraha baya la kichwa baada ya kugongana na beki David Luiz wa Arsenal katika mchuano wao wa awali wa EPL.
Kukosekana kwa Jimenez kulihisika pakubwa kambini mwa Wolves waliosalia kutegemea maarifa ya Adama Traore, Daniel Podence, Leander Dendoncker na Pedro Neto katika safu ya mbele. Hata hivyo, uthabiti wa Fabinho aliyeshirikiana vilivyo na Matip na Alexander-Arnold uliwabana kabisa wavamizi wa Wolves walioshindwa kumtatiza kipa chipukizi wa Liverpool, Caoimhin Kelleher aliyekuwa akiwajibishwa katika EPL kwa mara ya kwanza msimu huu.
Liverpool kwa sasa wameshinda mechi 31 na kuambulia sare mara moja katika jumla ya mechi 32 zilizopita za EPL katika uwanja wao wa nyumbani. Kutokana na michuano hiyo, wamefunga mabao 93 na nyavu zao kutikiswa na wapinzani mara 25 pekee.
Tangu Liverpool wavaane na Ajax ya Uholanzi katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba, mabingwa hao watetezi wa EPL wamefungwa mabao sita pekee kutokana na mechi 11 na wapinzani wameshindwa kuwafunga katika michuano sita. Mechi dhidi ya Ajax ilikuwa yao ya kwanza baada ya beki Virgil van Dijk kupata jeraha baya la goti dhidi ya Everton katika EPL.
Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Midtjylland ya Denmark kwenye UEFA mnamo Disemba 9, 2020 kabla ya kushuka dimbani kuchuana na Fulham kwenye EPL mnamo Disemba 13 uwanjai Craven Cottage. Kwa upande wao, Wolves wameratibiwa kuwa wenyeji wa Aston Villa uwanjani Molineux mnamo Disemba 12, 2020.