• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Gor Mahia kukutana sasa na CR Belouizdad ya Algeria katika CAF Champions League

Gor Mahia kukutana sasa na CR Belouizdad ya Algeria katika CAF Champions League

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya na washindi mara 19 wa kipute hicho, Gor Mahia watavaana sasa na CR Belouizdad ya Algeria katika raundi ya kwanza ya kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu huu.

Hii ni baada ya miamba hao wa Algeria kuwapokeza Al-Nasr ya Libya kichapo cha 2-0 mnamo Disemba 6, 2020 na kuwabandua kwenye hatua ya mchujo kwa jumla ya mabao 4-0.

Mabao ya Belouizdad katika mchuano wa mkondo wa pili yalifumwa wavuni na Chouaib Keddad katika dakika ya 16 kabla ya Salah Fekroune kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili. Mechi hiyo ilitandaziwa mjini Benghazi, Libya.

Kwa mujibu wa droo ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), mechi za mkondo wa kwanza katika raundi ijayo ya kipute hicho zitasakatwa kati ya Disemba 22-23, 2020 kabla ya marudiano kwa minajili ya mkondo wa pili kupigwa kati ya Januari 5-6, 2021.

Belouizdad ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Algeria. Taji hilo walilotia kapuni mnamo 2019-20 ndilo la kwanza tangu mwaka wa  2001 na saba katika historia ya kivumbi hicho.

Gor Mahia walisonga mbele kwenye kampeni za CAF msimu huu baada ya kuwabandua APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 4-3.

Miamba hao wa soka ya Kenya walipokezwa kichapo cha 2-1 jijini Kigali mnamo Novemba 28, 2020 kabla ya kusajili ushindi wa 3-1 katika mkondo wa pili uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Disemba 5, 2020.

Bao la pekee la Gor Mahia katika mkondo wa kwanza dhidi ya APR lilifumwa wavuni na Charles Momanyi huku wakifungiwa na Samuel Onyango, Sydney Ochieng na Nicholas Kipkirui katika mechi ya marudiano.

DROO YA CAF CHAMPIONS LEAGUE

CR Belouizdad (Algeria) na Gor Mahia (Kenya) 

Stade Malien (Mali) na Wydad Casablanca (Morocco)

Teungueth (Senegal) na Raja Casablanca (Morocco)

RC Abidjan (Ivory Coast) na Horoya AC (Guinea)

AS Sonidep (Nigeria) na Al Ahly (Misri, mabingwa watetezi)

Al Ahly Benghazi (Libya) na Esperance (Tunisia)

Gazelle (Chad) na Zamalek (Misri)

AS Bouenguidi (Gabon) na TP Mazembe (DR Congo)

Jwaneng Galaxy (Botswana) na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

Young Buffaloes (Swaziland) na V Club (DR Congo)

Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) na Primeiro Agosto (Angola)

Al Merrikh (Sudan) na Enyimba (Nigeria)

Asante Kotoko (Ghana) na Al Hilal (Sudan)

Mouloudia Alger (Algeria) na CS Sfaxien (Tunisia)

Nkana (Zambia) na Petro Atletico (Angola)

FC Platinum (Zimbabwe) na Simba SC (Tanzania)

You can share this post!

Kiwanda cha kuongezea ndizi thamani Kisii

Gaspo wafichua malengo yao ya msimu huu ligini baada ya...