Makala

SHINA LA UHAI: Mzigo wa HIV na Kansa ya mlango wa uzazi kwa wanawake

December 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 5

Na LEONARD ONYANGO

WAKATI wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Desemba 1, wiki iliyopita, watu jasiri wanaoishi na virusi vya HIV walitumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha Wakenya kwenda kupimwa ili kujua hali zao.

Miongoni mwa waliotoa uhamasisho huo ni Doreen Moraa ambaye anasema alizaliwa na virusi vya HIV zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Bi Moraa anataja HIV kuwa virusi ‘vidogo’ ambavyo havifai kushtua watu au kutumiwa kuwatenga na kubagua waathiriwa.

“Ninaita virusi vya HIV kuwa ‘mgeni wangu mdogo’ kwa sababu ni vidogo hata havionekani kwa macho. Niligundua kwamba watu walikuwa wanavipa nguvu nyingi kwa kuvitumia kuwabagua wengine,” anasema Bi Moraa.

Aligunduliwa kuwa na virusi vya HIV alipokuwa na umri wa miaka minane na kufikia sasa amekubali hali yake na anaishi maisha kawaida sawa na watu wengine wasiokuwa na virusi.

Naye, Mercy Wanjiku, 28, anasema kuwa aliamua kuweka wazi hali yake kuhusu HIV ili kuwapa matumaini Wakenya, haswa vijana, wanaoishi na virusi hivyo na wale wanaohofia kujitokeza kupimwa.

Anasema japo alizaliwa na virusi vya HIV, aligundua kwamba alikuwa ameathirika akiwa na umri wa miaka 13.

Mama yake aliyemwambukiza virusi hivyo akiwa tumboni, alifariki mnamo 2005, baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kansa ya mlango wa uzazi (cervical cancer).

“Wakati nilizaliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita, hakukuwa na elimu ya kutosha kuhusu namna ya kukinga mtoto aliye tumboni dhidi ya kuambukizwa HIV. Hivyo, simlaumu mama yangu,” anasema Bi Wanjiku.

Anasema kuwa aligundua kwamba alikuwa na virusi vya HIV baada ya kuugua mara kwa mara akiwa shuleni. “Mwalimu wangu alinishauri kwenda hospitalini. Nilipoenda nyumbani nilimwambia mama anipeleke hospitalini. Nilipimwa na mama alipoenda kuchukua matokeo, niliona uso wake umejawa na huzuni. Hapo ndipo nilijua kuwa kulikuwa na tatizo,” akasema.

Ripoti iliyotolewa na Programu ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukimwi na Magonjwa ya Zinaa (NASCOP) Desemba 1, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi, ilionyesha kuwa Wakenya milioni 1.5 wanaishi na virusi vya HIV.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 20,000 walifariki kutokana na maradhi yanayohusiana na Ukimwi mwaka jana.

Watu 41,000 wengi wao wakiwa wanawake na vijana wa chini ya umri wa miaka 24, walipatikana na HIV mwaka jana.

Ripoti inaonyesha kuwa kati ya watu milioni 1.5 walio na HIV, 943,000 ni wanawake.

Bi Moraa na Bi Wanjiku ni miongoni mwa asilimia 80 ya Wakenya milioni 1.5 wanaoishi na HIV, ambao wamekuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo, maarufu ARVs, kwa uaminifu.

Idadi ya watu wazima wanaotumia ARVs imeongezeka kutoka asilimia 64 mnamo 2008 hadi asilimia 80 mwaka huu.

Katika kipindi sawa, idadi ya watoto wanaotumia ARVs imeongezeka kutoka asilimia 18 hadi asilimia 70.

Huku tembe za ARVs zikiwa zimefanikiwa kuwezesha waathiriwa kuishi maisha ya kawaida, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la idadi ya wanawake walio na virusi vya HIV wanaopatwa na kansa ya mlango wa uzazi.

Mamake Moraa ni miongoni mwa wanawake wenye virusi vya HIV ambao wamefariki kutokana na kansa ya mlango wa uzazi.

Ripoti ya WHO iliyotolewa mwezi uliopita inaonyesha kuwa wanawake walio na HIV wako katika hatari ya kupatwa na kansa ya mlango wa uzazi mara sita zaidi ikilinganishwa na wenzao wasiokuwa na Ukimwi.

WHO linakadiria kwamba asilimia tano ya waathiriwa wa kansa ya mlango wa uzazi kote duniani wanaishi na HIV.

Lakini ripoti hiyo pia inakadiria kuwa karibu asilimia 30 ya wanawake walio na kansa ya mlango wa uzazi wanaishi na HIV humu nchini.

Aidha imeorodhesha Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yaliyo na idadi kubwa ya wanawake walio na HIV wanaougua kansa ya mlango wa uzazi.

Hiyo inatokana na uwepo wa visa vingi vya virusi vinavyosababisha maradhi ya zinaa (HPV)

WHO linaonya kuwa idadi ya wanawake wanaopatwa na kansa ya mlango wa uzazi itaongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Kenya iwapo serikali haitaongeza juhudi za kutoa chanjo kwa wasichana na kuwezesha akina mama kupata matibabu ya mapema.

Aidha linahimiza Kenya pamoja na mataifa mengineyo kutoa chanjo ya kuzuia HPV kwa angalau asilimia 90 ya wasichana wa kati ya umri wa miaka 10 na 14 kufikia 2030.

Who pia linataka serikali kuwezesha asilimia 90 ya wanawake kupata vipimo na matibabu ya kansa ya mlango wa uzazi ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo.

“Iwapo malengo hayo yataafikiwa, visa vipya vya maradhi ya kansa ya mlango wa uzazi vitapungua kwa asilimia 40 kote duniani,” linasema shirika la WHO.

Virusi vya HPV

Virusi vya HPV huchangia pakubwa kwa wanawake wanaoishi na virusi vya HIV kupatwa na kansa ya mlango wa uzazi.

Wataalamu wanasema kuwa miili ya wanaoishi na HIV hushindwa kukabiliana na virusi vya HPV ikilinganishwa na wenzao wasiokuwa na Ukimwi.

HIV pia hufanya kingamwili, maarufu CD4, kuwa dhaifu hivyo kusababisha HPV kulemea mwili.

Tafiti zimebaini kuwa wengi wa wanawake wanaopatwa na maradhi ya saratani ya mlango wa uzazi wana upungufu wa kinga za CD4.

Utafiti uliofanywa nchini Botswana ulibaini kuwa idadi kubwa ya wanawake wanaofariki kutokana na kansa ya mlango wa uzazi, wanaishi na HIV.

Kulingana na WHO, wanawake walio na HIV huambukizwa mara kwa mara HPV hata baada ya kutibiwa.

HPV ni kundi la virusi ambavyo huathiri ngozi na sehemu nyingine nyororo za mwili kama vile uke na uume. Virusi hivi huchangia pakubwa kwa kutokea kwa kansa ya koo, mdomo, sehemu ya kupitisha haja kubwa, uke na uume.

Kuna karibu aina 200 za virusi vya HPV. Takribani aina 40 huathiri maeneo ya sehemu nyeti na hatimaye vinaweza kusababisha magonjwa ya zinaa. HPV huenezwa kwa njia ya kujamiiana lakini pia mtu anaweza kuvipata kwa kugusana kimwili na mtu aliye navyo.

Karibu aina 13 za HPV husababisha saratani ya mlango wa uzazi, kwa mujibu wa wataalamu.

Takribani wanawake 5,250 hupatikana na kansa ya mlango wa uzazi humu nchini kila mwaka. Hiyo inamaanisha kuwa wanawake 14 hupatikana na maradhi hayo humu nchini kwa siku.

Aina hii ya kansa ni ya nne kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo miongoni mwa wanawake.

Kansa ya mlango wa uzazi huathiri zaidi wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 30, kulingana na WHO.

Mbali na HIV, mambo mengine yanayomweka mtu katika hatari kubwa ya kupatwa na HPV ni kushiriki mapenzi mapema katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, maradhi ya zinaa na uvutaji wa sigara.

Matibabu

Kansa ya mlango wa uzazi inaweza kuzuiliwa na hata kutibika iwapo mwathiriwa atapata matibabu mapema.

Mkuu wa Programu ya Kitaifa kuhusu Chanjo Dkt Collins Tabu, anashauri wanawake wanaoishi na HIV kupimwa kila mwaka ili kufahamu ikiwa wana kansa ya mlango wa mfuko wa uzazi au la.

“Mtu huwa haonyeshi dalili zozote baada ya kupata kansa ya mlango wa uzazi. Hivyo, vipimo vya mara kwa mara ni muhimu,” anasema.

Dkt Tabu anasema kuwa baada ya mwathiriwa kukaa kwa muda mrefu na maradhi hayo, huanza kutoa damu ukeni baada ya kushiriki ngono.

Australia inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza duniani kumaliza kansa ya mlango wa uzazi ndani ya miaka 20 ijayo kutokana na juhudi zake za kuhakikisha kuwa wanawake wanapimwa mara kwa mara na kupata matibabu ya mapema.

Serikali ya Australia pia imeimarisha juhudi za kutoa chanjo kwa wasichana wa kati ya umri wa miaka 10 na 14 ili kuzuia HPV.

Kenya ilizindua chanjo ya HPV mwaka jana inayolenga jumla ya wasichana 800,000 wa kati ya umri wa miaka 10 na 14.

Wataalamu wanasema kuwa kutoa chanjo kwa wasichana ambao hawajaanza kujiingiza katika mapenzi, kutasaidia pakubwa katika kumaliza virusi vya HPV na kansa ya mlango wa uzazi.

Kulingana na Dkt Tabu, asilimia 99 ya aina ya kansa zinazosababishwa na HPV zinaathiri wanawake.

Dkt Tabu anasema kuwa serikali itaelekeza juhudi zake kwa watoto wa kiume baada ya wasichana wote kupewa chanjo hiyo.

Virusi vya HPV vinaweza kusababisha kansa ya uume, mdomo na sehemu ya haja kubwa miongoni mwa wanaume.