Habari Mseto

Viongozi sasa wahofia hali ngumu ya kiuchumi nchini

December 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

JUHUDI za kutaka kufufua sekta ya sukari na sekta nyinginezo za uchumi katika ukanda wa Magharibi huenda zikakosa kuzaa matunda kufuatia janga la virusi vya corona na kuongezeka kwa mzigo wa madeni.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa na Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong, jana walionya kuwa hali ya kiuchumi itakuwa ngumu zaidi humu nchini huku wakisema kuwa nchi imelemewa na mzigo mzito wa madeni kwani sasa Kenya inadaiwa Sh8.4 trilioni.

Hiyo inamaanisha kuwa kila Mkenya anadaiwa karibu Sh170,000.

Viongozi hao walisema kuwa kuongezeka kwa deni hilo kumeathiri pakubwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Bw Mudavadi alisema kuwa huduma katika kaunti huenda zikatatizika kutokana na hatua ya Serikali ya Kitaifa kuchelewa kutoa fedha kwa serikali za ugatuzi.

“Serikali za Kaunti zimeshindwa kulipa wafanyakazi, shirika la kusambaza umeme (Kenya Power) linapata hasara kwa sababu baadhi ya wateja wake hawalipii huduma,” akasema Bw Mudavadi.

Aliwataka viongozi wa kidini kuombea taifa ili Mungu awezeshe Kenya kukabiliana na changamoto tele zilizosababishwa na deni kubwa ambalo limefanya serikali kupanga kuwatimua watumishi wake kadhaa.

Bw Mudavadi alisema kuwa wanafunzi kutoka familia maskini huenda wakakosa kuendelea na masomo yao ya vyuo vikuu kufuatia hatua ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) kupunguza kiasi cha fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wanafunzi.

“Pendekezo la kutaka kupunguza mikopo ya Helb ni tishio kwa elimu ya juu. Uamuzi huo unafaa kutupiliwa mbali,” akasema kiongozi wa ANC.

Gavana wa Busia, Bw Ojaamong alisema kuwa hatua ya serikali ya kitaifa kukosa kutoa fedha ndiyo husababisha migomo ya wafanyakazi katika kaunti mara kwa mara.

“Serikali za kaunti zilipokea fedha mara ya mwisho mnamo Agosti 2020,” akasema Bw Ojaamong ambaye anataka serikali kuingilia kati ili kuzuia mgomo wa wahudumu wa afya ambao unanukia.

Waziri Wamalwa alisema kuwa viongozi wa Magharibi wana kibarua kigumu kuhakikisha kuwa wanafufua sekta za sukari na kilimo cha pamba.

“Tunahitaji kufufua viwanda vya pamba katika Kaunti ya Busia na sekta ya sukari katika Kaunti za Kakamega na Bungoma. Viongozi wa Magharibi wanafaa kufikiria masuala yatakayofaidi wakazi badala ya kuzungumzia siasa za 2022. Tukiungana na kuzungumza kwa sauti moja, tutaweza kufufua uchumi wa eneo hili,” akasema.

Waziri wa Ugatuzi aliwataka viongozi wa Magharibi kuweka tofauti zao za kisiasa na ukabila kando na badala yake waungane na washughulikie miradi ya maendeleo kwa manufaa ya watu wote.