Afya: Kilio serikali zajikokota kusaidia
Na WACHIRA MWANGI
MASHIRIKA ya kijamii kutoka Pwani yameshutumu Serikali ya Kitaifa na Kaunti kwa kujikokota katika kumaliza migomo ya wahudumu wa afya ambayo imeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Muungano wa mashirika ya kijamii na mashirika ya kidini katika ukanda wa Pwani yaliitaka serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kushughulikia kwa haraka kero za wahudumu wa afya ili kuokoa maisha ya Wakenya wakati huu wa janga la virusi vya corona.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Zedekiah Atika, wanaharakati hao walitaka wakuu wa serikali ya kitaifa na kaunti kuelekeza juhudi zao katika kutatua changamoto zinazokumba sekta ya afya badala ya kuzunguka nchini wakihubiri Mpango wa Maridhiano (BBI).
“Tunasikitika kwamba serikali inaonekana kupuuza suala la afya ambalo linahusiana na haki za Wakenya. Wahudumu wa afya ambao wako katika mstari wa mbele katika kupambana na janga la virusi vya corona wanastahili kusikilizwa,” akasema Bw Atika.
Alishutumu serikali kwa kujaribu kutumia mbinu ya kugawanya wahudumu wa afya katika harakati za kusambaratisha migomo.
“Wauguzi na maafisa wa kliniki tayari wamegoma. Madaktari wametoa ilani ya siku 14 ili kuanza mgomo wao iwapo serikali haitatekeleza matakwa yao. Madaktari peke yao hawawezi kuendesha hospitali. Serikali ishughulikie malalamishi ya wahudumu wote wa afya kwa dharura.
“Tunafaa kuwapa wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya corona sawa na wanajeshi ambao wamepewa vifaa vya kutosha kupambana na maadui,” akasema Bw Atika.
Wanaharakati hao waliitaka Mamlaka ya Kusambaza Dawa na Vifaa vya Matibabu (Kemsa) kutoa vifaa vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi vya corona, maarufu PPEs.
Wahudumu wa afya wanataka kupewa PPEs na kulipwa mishahara yao mapema.
Wahudumu wa afya zaidi ya 2,200 wameambukizwa virusi vya corona na kati yao zaidi ya 30 wamefariki.
Wanaharakati hao pia walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kutimiza ahadi yake aliyotoa ya kuwanasa watu waliohusika na wizi wa mamilioni ya fedha zilizotengwa kupambana na janga la virusi vya corona.
Wagonjwa katika Kaunti ya Mombasa wamekuwa wakihangaika kwa wiki tatu sasa kufuatia mgomo wa madaktari. Huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Coast General zimetatizika kufuatia mgomo huo.
Mashirika ya kijamii yalimtaka Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho kuelekeza nguvu zake katika sekta ya afya kama alivyofanya baada ya kisa cha kwanza cha mwathiriwa wa virusi vya corona kuthibitishwa humu nchini mnamo Machi mwaka huu.