Habari

Sonko adai kamati ya maseneta 11 haitamtendea haki katika kuamua hatima yake

December 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amepinga vikali pendekezo kwamba mashtaka kwenye hoja ya kumtimua afisini yachambuliwe na Kamati maalum ya maseneta 11.

Akiongea Jumanne usiku dakika chache baada ya Kamati ya Kuratibu Shughuli ya Bunge la Seneti (SBC) kutoa pendekezo hilo, Sonko alisema anataka suala hilo lishughulikiwe na safu yote ya bunge la Seneti kwani “wanachama wa kamati maalum watashawishiwa na kuhongwa ili waniangushe.”

“Huu mkono wa kamati maalum siutaki kwa sababu hautahakikisha haki imetendekeza. Wanachama hao 11 wataingiliwa na maadui wangu wa kisiasa ambao ndio walidhamini hoja hiyo ambayo ni kinyume na Katiba,” Bw Sonko akasema kupitia akaunti yake ya twitter

Mnamo Jumanne alasiri SBC ilipendekeza kwamba hoja ya kumwondoa afisini Gavana Sonko ichanganuliwe na kamati maalum ya maseneta 11.

Spika wa bunge hilo Kenneth Lusaka ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo alithibitisha kuwa wanachama wa kamati hiyo wameunga mkono mkondo huo wa kushughulikia mashtaka dhidi ya gavana huyo “ili kuhakikisha haki imetendeka kwa pande zote; bunge la Nairobi na Gavana Sonko.”

“Wanachama wa SBC wameamua mfumo wa kamati utumike. Kwa hivyo, kesho (leo Jumatano) hoja itawasilishwa kuhusu pendekezo hilo na kupigiwa kura na maseneta wote,” Bw Lusaka akasema.

Naye kiranja wa wachache Mutula Kilonzo Junior alisema japo SBC imependekeza suala hilo lishughulikiwe kupitia kamati maalum, kamati ya maseneta wote bado ndiyo itakuwa na usemi wa mwisho kuhusu suala hilo.

“Sasa ni wajibu kikao cha bunge lote linalokutana kesho (leo Jumatano, Desemba 9, 2020) alasiri kuamua ikiwa mfumo huo unafaa au la.” akasema.

Mkondo huo wa kamati ulitumiwa Juni 2020 wakati wa kushughulikiwa kwa hoja ya kumtimua afisini Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

Baada ya siku 10 kama hiyo iliyoongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ilimwondolea lawama gavana huyo japo ikasema kuwa madai ua ufisadi dhidi yake yalipasa kushughulikiwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).