Polisi ashtakiwa kwa kumjeruhi mwenzake
Na RICHARD MUNGUTI
AFISA wa polisi ameshtakiwa kwa kumdunga kisu na kumpa majeraha ya kudumu afisa mwenzake waliyezozania mwanamke huku polisi mwingine akishtakiwa kumvunja mkono mwenzake akitekeleza sheria za kafyu mbele ya mke wake.
Maafisa hao Konstebo Dickson Mugo Kabita na Konstebo Evans Mithika walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Bi Martha Mutuku wakikabiliwa na mashtaka ya kuwajeruhi wahasiriwa na kuwapa majeraha ya kudumu.
Katika kesi ya Bw Kabita mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda kwamba mshtakiwa huyo na mwenzake Konstebo Samuel Kiarie Muhuni walikuwa wanabugia pombe katika kilabu kimoja mtaani Kariokor walipozozana juu ya kidosho.
Bw Gikunda alisema maafisa hao wa kudumisha usalama walikabiliana vikali huku kila mmoja akijaribu kumuwahi mwenzake ndipo ahepe na Bi Kisura huyo.
Konstebo Kabita alimfuma kisu tumboni mlalamishi ambaye alipiga kamsa na kuzirai baada ya muda kidogo.
“Mshtakiwa aliyekuwa amejihami kwa kisu alimdunga tumboni mwenzake katika hali ya kumlemaza ndipo apate fursa ya kuhepa na mwanadada huyo wakaponde raha,” Bw Gikunda alimweleza hakimu mkuu Bi Mutuku huku akipinga mshtakiwa akiachiliwa kwa usalama.
Bw Gikunda alieleza mahakama mlalamishi angali katika hali mahututi na “huenda shtaka likabadilika.”
Pia alisema mshtakiwa akiachiliwa sasa kwa dhamana atawavuruga mashahidi.
“Ukimwachilia mshtakiwa kwa sasa kwa dhamana atavuruga ushahidi ikitiliwa maanani angali anahudumu katika idara ya polisi,” Bi Gikunda alisema.
Bi Mutuku aliamuru mshtakiwa azuiliwe ndipo afisa anayechunguza kesi hiyo akamilishe mahojiano na mashahidi kisha mshtakiwa arudishwe kortini wiki ijayo kwa maagizo zaidi.
Maafisa hao wawili huhudumu katika kituo cha Polisi cha Kariokor
Wakati huo huo Konst Mithika alishtakiwa kwa kumpiga na kumjeruhi Inspekta Bernard Mochama.
Kwa mujibu wa Bw Gikunda, Insp Mochama alikuwa anarudi nyumbani nao washtakiwa walikuwa wanashika doria katika eneo la Mawe Mbili Ruai kaunti ya Nairobi.
Insp Mochama alikutana na mshtakiwa akiwa ameandamana maafisa wengine wa polisi wakishika doria kutekeleza sheria za kafyu.
Insp Mochama alikuwa ameabiri boda boda kusudi asichelewe na kupatwa na masaa ya kafyu akiwa nje.
Mshtakiwa kisha wakamsimamisha na kumtaka ajitambulishe. Aliwapa kitambulisho cha Idara ya Polisi lakini hawakuridhika.
“Wewe ni nani? Leta kitambulisho kisha ujieleze,” Bw Gikunda alisema.
Mshtakiwa alipohisi atateswa alitoroka akielekea nyumbani kwake.
Mahakama ilielezwa mshtakiwa na mwenzake walimfuata unyounyo Bw Mochama na kumpata akiwa anasubiri lango lifunguliwe.
“Mlalamishi alipata kichapo cha nguruwe mbele ya mkewe aliyekuwa ametoka kwa nyumba kumfungulia lango la nje ya ploti,”alisema Bw Gikunda.
Mahakama ilielezwa majirani walijmwokoa mlalamishi kisha wakampeleka katika Kituo cha Polisi cha Njiru na kulalamika.
Kesi hizo mbili zitatajwa Desemba 15, 2020 kwa maagizo zaidi.