• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
JUNI 3: Tarehe ambayo Kenya itasafirisha mafuta ya kwanza kutoka Turkana

JUNI 3: Tarehe ambayo Kenya itasafirisha mafuta ya kwanza kutoka Turkana

Na BERNARDINE MUTANU

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua ziara ya kwanza ya kusafirisha mafuta kutoka Lokichar, Kaunti ya Turkana, Juni 3.

Katika taarifa Jumatano, Ikulu ilitangaza kuwa siku hiyo iliafikiwa baada ya mkutano na washikadau wanaochimba mafuta Lokichar.

Kampuni hizo ni Tullow Oil, Africa Oil na Total. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi kutoka Turkana akiwemo Gavana Josphat Nanok na Waziri wa Madini John Munyes.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hatua hiyo na utekelezaji wa mpango wa majaribio ya kuchimba mafuta(EOPS) utakuwa ni mwanzo wa sekta mpya katika uchumi wa Kenya.

“Tuko tayari kuanza, hii ni muhimu sana kwa taifa letu na kwa jamii husika,” alisema rais wakati wa mkutano huo.

Wiki iliyopita, Ikulu ilisema kuwa shughuli hiyo ingetekelezwa Juni 1, lakini tarehe hiyo ikabadilishwa. Kampuni hizo zitaendelea kuchimba mafuta katika visima vilivyokuwa na zitakuwa zinatoa mapipa 2,000 ya mafuta kwa siku.

Mafuta hayo yatasafirishwa kwa barabara kutoka Turkana hadi Mombasa katika Kampuni ya Mafuta (Kenya Petroleum Refinaries) ambako yatakusanywa kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Mwaka wa 2015, Tullow Oil iliweza kuchimba mapipa 70,000 wakati wa kufanyia majaribio mradi huo.

You can share this post!

Kesi dhidi ya Wazir Chacha yaunganishwa na nyingine

Lionesses kukabana na Senegal raga

adminleo