Wabunge kunyolewa Sh1 milioni kila mmoja
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA imeagiza wabunge na maseneta warudishe jumla ya Sh357 milioni walizojiongezea kama marupurupu ya nyumba kuanzia 2018 kinyume cha sheria.
Punde tu baada ya Majaji Pauline Nyamweya, Weldon Korir na John Mativo kuamuru wabunge na maseneta hao warudishe pesa hizo, Karani wa Bunge Michael Sialai alisema kila mbunge na seneta atakatwa Sh1 milioni.
Bw Sialai alisema mahakama iliposimamisha malipo hayo, kila mbunge alikuwa tayari amepokea Sh1 milioni.
Mahakama iliamuru pesa hizo zirudishwe katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kesi hiyo iliwasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah.
Wakiamuru wabunge na maseneta 416 warudishe fedha hizo, majaji hao watatu waliiokosoa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kwa kujitwika jukumu lisilo lake.
Majaji hao walisema jukumu la kuamua mishahara na marupurupu itakayolipwa watumishi na maafisa wa umma limepewa Tume ya SRC.
“Ni SRC tu iliyopewa jukumu la kuamua mishahara na marupurupu yanayolipwa maafisa wa umma. Wabunge walijitwika jukumu lisilo lao. Hatua hiyo ni kinyume cha sheria,” waliamua majaji hao.
Majaji walisema katiba haijaipa PSC jukumu la kuamua kiwango cha mshahara wa wabunge ama wa maseneta watakachopokea.
Pia walisema PSC haiwezi kuamua mshahara utakaopewa wafanyakazi wanaohudumu katika idara ya bunge.
Majaji hao walisema jukumu la kifedha ambalo limetunukiwa PSC ni kutengeneza bajeti yake.
“Mahakama imefikia uamuzi kuwa mamlaka ya kila asasi ya serikali lazima iongozwe na vipengee vya sheria na Katiba. PSC haijapewa mamlaka hayo kisheria kuamua mshahara na marupurupu ya nyumba ya wabunge na maseneta,” walisema majaji hao.
Mahakama hiyo ilisema SRC ilitekeleza ipasavyo jukumu lake ilipoamuru wabunge na maseneta wasilipwe marupurupu hayo.