Habari Mseto

Msitulaumu kwa mafuriko ya Tana River – KenGen

May 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya kuzalisha umeme (KenGen) imejitetea kuhusiana na madai kwamba iliachalia maji kutoka kwa mabwawa yake na kusababisha mafuriko maeneo ya Garissa.

Meneja wa uhusiano mwema Grace Chepkwony Alhamisi alisema KenGen haikufaa kulaumiwa kwa sababu ya mafuriko Garissa na Tana River.

Alisema hayo alipokutana na wanahabari katika Kaunti ya Tana River. Alieleza kuwa mafuriko yalianza kushuhudiwa Tana River kabla ya Bwawa la Masinga kujaa.

Meneja huyo alisema KenGen iliwafahamisha wakazi wa maeneo hayo kuhusiana na ongezeko la maji katika bwawa hilo na uwezo wa kuvunja kingo zake kwa sababu ya mvua kubwa nchini.

Bi Chepkwony alisema haingekuwa mabwawa hayo saba ya kuzalisha umeme katika Mto wa Tana, hali ingekuwa mbaya zaidi.