Michezo

Spurs wapepeta Antwerp katika Europa League huku Mourinho akisema ameshindwa kuridhisha kila mmojawapo wa wachezaji wake

December 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba haiwezekani kuridhisha kila mchezaji baada ya kikosi chake kilichofanyiwa mabadiliko mengi kupepeta Royal Antwerp ya Ubelgiji 2-0 mnamo Disemba 10, 2020.

Ushindi wa Spurs uliwawezesha kufuzu kwa hatua ya 32-bora ya Europa League wakiwa kileleni mwa Kundi J.

Mourinho aliwapumzisha wanasoka wengi ambao amekuwa akiwategemea kwenye kikosi cha kwanza katika EPL wakati wa mechi hiyo dhidi ya Antwerp. Miongoni mwa waliokosa kunogesha mchuano huo ni Harry Kane na Son Heung-min. Kutokuwepo kwao kulimpa fursa ya kuchezesha Gareth Bale, Carlos Vinicius na Harry Winks.

Vinicius aliwaweka Spurs uongozini katika dakika ya 57 baada ya kipa Alireza Beiranvand kumnyima Bale nafasi kadhaa za kufunga.

Giovani lo Celso alifunga bao la pili la Spurs katika dakika ya 71 kabla ya kuondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mabadiliko yaliyofanywa na Mourinho katika kikosi chake yalikera baadhi ya wachezaji wa Spurs, akiwemo Harry Winks aliyeondoka kabisa uwanjani baada ya kuondolewa ugani katika dakika ya 67.

Dele Alli naye aliondoka kwenye eneo walikokuwa wamekalia wachezaji wa akiba wa Spurs baada ya Mourinho kufanya mabadiliko ya tano na ya mwisho katika kipindi cha pili.

“Siwezi nikamridhisha kila mtu kambini. Kunao watakaopata nafasi ya kucheza katika baadhi ya mechi na wengine watakosa,” akatanguliza Mourinho ambaye ni raia wa Ureno.

“Nadhani baadhi ya wachezaji wangu wa Spurs wanakereka kwa sababu tunashinda, sidhani wanaudhika kwa sababu hawachezi katika kila mchuano,” akasema.

“Kila mchezaji aliyeondoka uwanjani walifanya hivyo kwa sababu niliwaeleza waende waoge kwa maji moto kwa kuwa kulikuwa na mzizimo na baridi kali. Baadhi waliamua kwenye na wengine wakasalia kwenye eneo la wachezaji wa akiba,” akaongeza.

“Ni nadra sana upate kikosi kinachoridhisha kila mchezaji. Ukienda katika kila timu, wanasoka ambao hawachezeshwi katika kila mchuano hawana furaha,” akaeleza.

Alli na Winks wamechezeshwa na Spurs mara nne pekee kila mmoja hadi kufikia sasa msimu huu. Mara ya mwisho kwa Alli kuwajibishwa na Spurs ilikuwa katika mechi ya kwanza ya kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Everton. Kwa upande wake, Winks alichezeshwa mara ya mwisho mnamo Septemba 2020.