Habari Mseto

Kaunti 13 kuvamiwa na nzige tena – Katibu

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI imeonya kuhusu uvamizi mwingine wa nzige wa jangwani katika kaunti 13 huku ikianzisha mikakati kabambe ya kukabiliana na wadudu hao ikiwemo utumizi wa ndege, helikopta na kemikali za kuwaangamiza.

Katibu Mkuu wa Kilimo Prof Hamadi Boga alisema kuwa ramani zao zinaonyesha kuwa nzige hao wameongezeka katika nchi za Somalia, Ethiopia na Yemen na sasa wanaingia kwa kasi humu nchini kufikia wikendi hii.

Wizara ya kilimo inafanya kazi pamoja na kaunti na mashirika ya kimataifa ili kukabiliana na nzige hao vilivyo.

Katibu huyo ameonya baadhi ya nzige hao wamewasili humu nchini wakisubiri wenzao kuvamia.

Hata hivyo, Prof Boga alisema kuwa tayari wameanza kupeleka vifaa vya kukabiliana na wadudu hao. Ramani yao inaonyesha kuwa wadudu hao huenda wakavamia kaunti za Mandera, Wajir, Marsabit, Isiolo, Garissa, Tana River, Turkana, Tharaka Nithi, Embu, Meru, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Pokot kuanzia wikendi hii.

“Hawa ni wadudu wanaoruka katika sehemu tambarare, hawawezi kupanda milima. Ramani na utabiri kutoka Shirika la Chakula na Kilimo duniani inaonyesha kuwa idadi ya nzige imeongezeka na wataingia humu nchini kuanzia wikendi hii. Hata hivyo eneo la Pwani litashuhudia uvamizi wa kiasi cha chini huku wengi wa nzige hao wakitarajiwa eneo la Kati na Kaskazini mwa Kenya. Idadi ndogo itaelekea nchini Tanzania na kidogo wakisalia kaunti ya Taita Taveta kwani upepo unavuma kuelekea nchi jirani na huenda wakaathirika na uvamizi wa wadudu hao,” alionya Prof Boga.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio, katibu huyo ameelezea wasiwasi wake iwapo wadudu hao watavamia kaunti za Samburu, Marsabit, Isiolo na Turkana itakuwa hatari kwani ni sehemu wanapoweza kuzaana kwa haraka kutokana na hali ya kaunti hizo.

“Hii ni kwa sababu watakuwa wakielekea Ethiopia na upepo unapovuma utawaregesha Kenya. Hata hivyo, tumeweka mikakati kabambe kukabiliana nao,” alisisitiza katibu.

Serikali tayari imetenga vituo vinane kusaidia kudhibiti uvamizi wa nzige hao. Vituo hivyo viko katika eneo la Witu, Wajir, Mandera, Turkana, Masinga, Samburu, Marsabit na Isiolo na dawa za kutosha, ndege tatu za kunyinyiza dawa, helikopta tatu, zaidi ya magari 50 na vijana kutoka shirika la huduma kwa vijana NYS.

Katibu huyo alisema serikali itakodisha magari zaidi na pikipiki kuwasaidia kuingia misituni kutafuta nzige hao. Vijana wa NYS pia watatumwa katika vituo hivyo wakishirikiana na serikali za kaunti na ya kitaifa kukabiliana na nzige hao.

Katibu wa kilimo alisema kuwa serikali itanyunyizia dawa kutumia ndege na hata magari.

Prof Boga alisema wanatumia dawa ya wadudu aina ya synthetic pyrethroid kukabiliana na wadudu hao ambayo ina madhara ya chini kwa mazingira huku akiendelea kulaumu vita vinavyoendelea Somalia kwa uvamizi humu nchini.