• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Aibu Harambee Stars kuadhibiwa nyumbani na Swaziland

Aibu Harambee Stars kuadhibiwa nyumbani na Swaziland

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars iliwakosa tegemeo Victor Wanyama na Michael Olunga, huku ikilemewa 1-0 na Swaziland katika mechi ya kirafiki uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Kiungo wa Tottenham Hotspur, Wanyama, alijiondoa kushiriki mechi za kirafiki dhidi ya Swaziland (Mei 25) na Equatorial Guinea (Mei 28) akisema anafuata ushauri kutoka kwa klabu hiyo yake ili aweze kupona kabisa jeraha la goti lililomsumbua kwa miezi minne msimu 2017-2018.

Olunga, ambaye kandarasi yake ya mkopo wa msimu mmoja katika klabu ya Girona nchini Uhispania kutoka Zhicheng Hengfeng nchini Uchina itatamatika Juni 30, aliomba ruhusa asijumuishwe kutokana na majukumu ya klabu.

Mshambuliaji huyu amekuwa akitegemwa sana kupata mabao. Alitikisa nyavu Kenya ilipotoka 1-1 dhidi ya Uganda katika mechi ya kirafiki Machi 23, 2017 na kusukuma wavuni mabao mawili katika mechi nyingine ya kujipima nguvu ambayo Stars ilikanyaga DR Congo 2-1 Machi 26, 2017.

Pia alipachika bao la kufutia machozi dhidi ya Sierra Leone katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, ambayo Stars ilipoteza 2-1 Juni 10, 2017.

Olunga aliona lango katika mechi za kirafiki ambayo Iraq ilishinda 2-1 Oktoba 5, 2017.

Katika mechi yake ya mwisho, Olunga alijaza kimiani bao moja, huku Kenya ikibwagwa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) hapo Machi 27, 2018. Mchuano huu pia ulikuwa wa kirafiki.

Stars, ambayo ilizaba Swaziland 2-0 zilipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 2013, ilipoteza 1-0 Ijumaa kupitia bao la mshambuliaji Barry Steenkamp. Lilipatikana dakika ya 78.

Kenya inaorodheshwa nambari 111 duniani nayo Swaziland inashikilia nafasi ya 131. Inatarajiwa kuporomoka kwenye viwango bora vya dunia vitakapotangazwa Juni 7.

Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Kenya wanasalia bila ushindi mwaka 2018. Walitoka sare ya 2-2 dhidi ya Comoros na kuzabwa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati wa mechi za kimataifa mwezi Machi.

Vijana wa Migne watapimana nguvu na nambari 145 duniani Equatorial Guinea hapo Jumatatu. Wataelekea mjini Mumbai kwa mashindano ya mwaliko ya Hero Intercontinental yatakayokutanisha India (wenyeji), Kenya, New Zealand na Chinese Taipei.

Stars inatumia michuano hii kujiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019. Kenya imekutanishwa na Ghana, Sierra Leone na Ethiopia katika mechi za Kundi F za kuingia AFCON. Ilipepetwa 2-1 na Sierra Leone katika mechi ya kwanza mwaka jana. Itaalika Black Stars ya Ghana mnamo Septemba 7, izuru Ethiopia (Oktoba 10), ialike Ethiopia (Oktoba 13) na kufunga mwaka huu dhidi ya Sierra Leone hapa nchini Novemba 16.

Vikosi:

Kenya: Wachezaji 11 wa kwanza – Boniface Oluoch (kipa), Jockins Atudo (nahodha), Mike Kibwage, Eric Ouma, Joash Onyango, Duncan Otieno, Patillah Omotto, Philemon Otieno, Francis Kahata, Whyvonne Isuza na Ovella Ochieng’; Wachezaji wa akiba – Patrick Matasi (kipa), Timothy Odhiambo (kipa), Humphrey Mieno, Marvin Omondi, Chrispin Oduor, Jafari Owiti, Pistone Mutamba, Musa Mohammed, Vincent Wasambo, Harun Shakava, Timothy Otieno na Bolton Omwenga.

Swaziland: Wachezaji 11 wa kwanza – Sandanezwe Mathabela, Lindo Mkhonta, Wandile Maseko, Banele Dlamini, Siboniso Ngwenya, Mandla Palma, Xolani Sibandze, Njabulo Ndlovu, Barry Steenkamp, Felix Bendenhorst na Tony Tsabedze; Wachezaji wa akiba – Nhlanhla Gwebu, Phumani Dlamini, Sihlangu Mkhwanazi, Zweli Nxumalo, Wonder Nhleko, Sifiso Mazibuko, Bonginkosi Dlamini, Phiwayinkosi Dlamini na Musa Dlamini.

You can share this post!

Wanaharakati wakamatwa kwa kupinga mradi wa makaa ya mawe

Sina tamaa ya kuhamia Liverpool wala Man United –...

adminleo