Habari Mseto

Uhuru sasa awataka machifu kuhakikisha watoto wanarejea shuleni

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewaamuru machifu na manaibu wao kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanarejea shuleni Januari 4 hapo mwakani.

Akiongea wakati wa sherehe za kitaifa za Jamhuri Dei katika uwanja wa Nyayo Jumamosi, Rais alisema hakuna mtoto anafaa kukosa kuhudhuria shule kuanzia Januari zitakapofunguliwa baada ya kufungwa kwa miezi tisa kutokana na janga la corona.

“Nawaamuru machifu wote na manaibu wote kuzunguka katika maeneo yao na kuhakikisha kuwa watoto wote wamerejea shule. Hatutaki kusikia kwamba kuna watoto ambao watasalia manyumbani kuanzia Januari 4. Ni haki ya kila mtoto kupata masomo,” akasema.

Rais Kenyatta pia aliwataka wazazi kuhakikisha kuwa wanawanunulia watoto wao mahitaji ya shule mwaka ujao, akiwaonya dhidi ya kutumia fedha zote katika sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Sherehekeeni Krismasi na Mwaka Mpya lakini mkumbuke kuwanunulia watoto wetu mahitaji yao ya shule. Msimalize pesa zote kwenye karamu na anasa,” akasema.

Rais Kenyatta alisema kuwa serikali inatatilia maanani usalama wa wanafunzi watakarejea shuleni, shughuli ambayo alisema itasimamiwa na Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na ile ya Usalama wa Ndani.

Alisema serikali kupitia Wizara za Elimu na Afya imebuni kanuni mahsusi itakayotumiwa kudhibiti usambao wa virusi vya corona shule zitakapofunguliwa.

“Tunataka kuhakikisha kuwa watoto wanasoma katika mazingira salama. Kwa hivyo, wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote wa shule wahakikishe kuwa wanavalia barakoa kila mara na kunawa mikono nyakati zote. Serikali itasambaza barakoa kwa watoto kutaka jamii masikini ambao watatambuliwa na walimu wao,” Rais Kenyatta akasema.

Kenya imekuwa ikiandikishwa kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vya corona tangu Oktoba serikali ilipowaruhusu wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kurejelea masomo ya kawaida.

Idadi ya wagonjwa wanaofariki pia imeongezeka miongoni mwao wakiwa walimu na wafanyakazi wa shule mbalimbali. Kufikia Jumamosi zaidi ya wagonjwa 1,500 walikuwa wameangamizwa na Covid-19 huku idadi jumla ya maambukizi ikiwa zaidi ya 90,000.