• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
TAHARIRI: Shirikisho la FKF linaficha nini?

TAHARIRI: Shirikisho la FKF linaficha nini?

KITENGO CHA UHARIRI

NI ukiukaji mkubwa wa uhuru wa wanahabari kwa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kuwazuia waandishi kufanya kazi yao ya kufuatilia mechi.

Siku ya Jumamosi, FKF iliwazuia wanahabari kufuatilia mechi ya Gor Mahia dhidi ya Ulinzi Stars katika uga wa Nyayo. Wanahabari wa Shirika la NMG walikuwa kati ya waliozuiwa na polisi kuingia kwenye uga huo bila kupewa sababu zozote maalum.

Kando na hayo, FKF ilionyesha mapendeleo kwa kuruhusu chombo kimoja tu cha habari nchini, ambacho kina mkataba na shirikisho hilo, kupeperusha mechi hiyo.

Hii si mara ya kwanza ambapo wanahabari wanahangaishwa kufuatilia mechi kutokana na agizo la FKF, ambayo iko katika mvutano na baadhi ya klabu nchini ambazo zimekataa kutia saini dili ya kampuni ya StarTimes ya upeperushaji wa mechi za Ligi Kuu (KPL).

Shirikisho hilo tayari limetimua Zoo Kericho na Mathare United kwenye ligi na linatarajiwa kuchukua hatua hiyo dhidi ya Gor Mahia na Ulinzi Stars wiki hii, iwapo klabu hizo mbili hazitaweka saini zao.

Ingawa hivyo, si vyema kwa Rais wa FKF Nick Mwendwa na kundi lake kuwaadhibu wanahabari wasio na hatia kwa sababu ya mvutano baina yake na klabu wala kwa kuanika mabaya yanayotokea katika utawala wake.

Wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Afrika (CAF) kati ya Gor Mahia na APR ya Rwanda mnamo Desemba 5, baadhi ya wanahabari pia walizuiwa kufuatilia mtanange huo.

FKF inadaiwa imekataa kuwapa vitambulisho maalum vya kuruhusu wanahabari kuingia uwanjani, eti kwa sababu wamekuwa wakikashifu uongozi wake kwenye vyombo vya habari hususan kuelekea uchaguzi wa shirikisho ulioandaliwa mwezi jana ambapo Mwendwa alichaguliwa kwa awamu ya pili ya uongozi.

Hata katika ligi zilizoendelea za bara Ulaya, ambazo ni maarufu sana miongoni mwa mashabiki hapa Kenya, mashirikisho ya soka hayaingilii kazi ya wanahabari hata yanapokosolewa kwani ni kwa kufichua maovu ambapo soka yao imelainishwa na kunawiri.

FKF itakuwa ikijichimbia shimo ikiwa inataka tu wanahabari waripoti ‘mazuri’ bila kuikosoa. Kosa sio kosa, bali ni kurudia.

Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) linafaa kuingilia kati suala hili na kushinikiza usimamizi wa FKF kuruhusu wanahabari kufanya kazi yao sio kuwahangaisha kwani hilo halifai kamwe katika karne hii.

MCK ichukua hatua dhidi ya usimamizi wa FKF ambao umedhihirisha kuwa hautaki kukosolewa huku wakitumia uchaguzi ulioandaliwa mwezi uliopita kuadhibu wanahabari walioandika makala ya kukosoa utawala wa Mwendwa.

You can share this post!

Masaibu ya wanahabari UG uchaguzi ukijongea

ODONGO: Viongozi hawafanyii raia hisani kutekeleza miradi