Makala

SHINA LA UHAI: Baada ya dhiki ya miaka 13, ‘uboho mpya’ ukampa faraja?

December 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PAULINE ONGAJI

KWA miaka 13 amekuwa akipambana na maradhi ya selimundu (sickle cell disease).

Ni ugonjwa ambao umeathiri pakubwa maisha ya Karen Mukabi, 17, mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka eneo la Lurambi, Kaunti ya Kakamega.

Tangu mwaka wa 2007 alipogundulika kuugua maradhi haya, wakati huo akiwa na miaka saba, hali haijakuwa shwari sio tu kiafya, bali pia kimasomo.

“Huwezi tabiri ni lini au ni wakati upi ambapo maradhi haya yatachochea ishara kali mwilini mwake, suala ambalo husababisha ziara za ghafla hospitalini kila wakati. Hii mara nyingi huathiri ratiba yake kimasomo,” aeleza Eunice Yeswa, mamake Mukabi.

Isitoshe, ni ugonjwa ambao umekuwa mzigo mkubwa wa kifedha kwa familia hii.

“Kwa miaka hii yote amekuwa akipokea matibabu mbalimbali, kama vile kudungwa sindano mishipani na kwenye misuli ili kudhibiti hali hii,” aeleza

Ni shughuli ambayo imewagharimu kitita kikubwa cha pesa.

“Kuna wakati ambapo anaweza pokea matibabu kila wiki, kila mwezi au mara mbili kwa mwezi, na kila wakati anaposhughulikiwa inanigharimu kati ya Sh1,500 na Sh55,000,” anasema.

Kulingana na Bi Yeswa, miaka hii 13 imekuwa ya dhiki na wasiwasi huku ugonjwa huu ukimfyonza sio tu kifedha, bali pia kisaikolojia.

Lakini huenda matatizo ya familia hii yakafikia kikomo hivi karibuni, ikiwa azma yao ya kutafuta tiba ya kudumu ng’ambo itatimia.

Bi Yeswa anasema kwamba baada ya kutafuta ushauri tofauti, ameamua kwamba bintiye awe mmoja wa watu wachache nchini, wanaosafiri ng’ambo kwenda kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza uboho, yaani Bone Marrow Transplant (BMT).

“Nilipata fursa ya kuzungumza na wataalamu kadha wa kadha, vile vile mwathiriwa wa ugonjwa huu aliyepona baada ya kufanyiwa utaratibu huo nchini India, na hapo nikaamua kwamba badala ya kusumbuka kila wakati kutokana na harakati za kudhibiti hali hii, basi tuchukue hiyo hatua ya kupata tiba ya kudumu,” aeleza.

Kwa hivyo shughuli za kumpeleka Mukabi nchini India kwa matibabu ziko mbioni, huku msichana huyu akitarajiwa kupandikizwa uboho kutoka kwa nduguye mdogo.

Kulingana na Dkt Satya Prakash Yadav, mkurugenzi wa idara ya matibabu ya kansa ya damu na upasuaji wa kupandikiza tishu za mifupa katika hospitali ya Medanta, Gurgaon- India, kwa kawaida watoto wote wanaougua maradhi ya selimundu wanapaswa kupewa dawa ya Hydroxyurea na kushughulikiwa ipasavyo.

“Mara nyingi hali ya kiafya huimarika baadaye pasipo kuhitaji upandikizaji uboho (BMT). Lakini kuna wale ambao hali yao haiimariki licha ya kupewa tiba ya Hydroxyurea, na hapa ndipo upasuaji wa BMT unahitajika,” aeleza.

Hospitali ya Medanta hufanya kati ya BMT 50 na 60, miongoni mwazo zikiwa kati ya 5-6 za kutibu selimundu.

Kwa hivyo upandikizaji uboho unahusisha nini?

Tiba hii huhusisha kubadilisha uboho kwenye mifupa (bone marrow) na kuweka mwingine. Uboho waweza kuwa ni wa kutoka kwa mfupa wa mwathiriwa (autologous) au kutoka kwa mtu mwingine (allogeneic).

“Utaratibu wa autologous BMT unatumika kutibu maradhi kama vile lymphoma, myeloma, uvimbe tofauti miongoni mwa watoto kama vile Neuroblastoma, Relapsed Ewing’s and Wilms Tumor, Medulloblastoma na kadhalila. Allogeneic BMT inatumika kutibu leukemia/lymphoma, Thalassemia, anemia selimundu, matatizo ya kinga mwilini na matatizo ya kimetaboli,” aeleza.

Kulingana na Dkt Prakash, allogeneic BMT ndio suluhisho la kipekee la kudumu kutibu maradhi ya selimundu, huku wanaofanyiwa upasuaji huu wakiwa na uwezekano wa kati ya 80-90% wa kupona kabisa.

“Ikiwa uboho utakaopandikizwa unatoka kwa ndugu wa mwathiriwa na unaambatana kabisa, basi uwezekano wa kupona baada ya upasuaji ni 90%. Ikiwa bidhaa hii inatoka kwa jamaa ya mwathiriwa (ndugu au mzazi) ambapo uboho unaambatana kwa kiwango nusu tu, basi uwezekano wa kupona kabisa ni 80%. Na endapo utatoka kwa mtu asiye na uhusiano wa kifamilia, basi uwezekano wa kupona ni 70 %.”

Mukabi, ana bahati kwamba ni nduguye mdogo aliyepatikana na uboho unaoambatana na wake.

Lakini kuna tatizo. Hapa nchini hakuna hospitali inayofanya upasuaji huu, suala ambalo limewalazimu wanaohitaji huduma hii kuisaka ng’ambo. Na hii imefanya iwe ghali hata zaidi kwa wanaosafiri ng’ambo kwenda kuhudumiwa.

Kwa mfano, kwa sasa familia ya Mukabi inahitajika kuwa na takriban Sh6.5 milioni, ikijumlisha gharama ya usafiri, ili kuhakikisha kwamba binti yao anapokea matibabu na kushughulikiwa kikamilifu kabla ya kurejea nchini.

“Hatuna pesa kabisa na tunategemea mikopo vile vile misaada ambapo tayari tunaendelea kuchanga pesa,” aeleza Bi Yeswa.

Huku familia hii ikiendelea kusaka fedha za matibabu nchini India, takwimu zinaonyesha kwamba hapa nchini, asilimia 90 ya watoto wengi wanaougua selimundu hufa kabla ya kutimu miaka mitano.

Barani Afrika, kati ya asilimia 50- 90 ya watoto wanaozaliwa na maradhi haya, hufa kabla ya kutimu miaka mitano huku sababu kuu ikiwa mataifa haya husika kutokuwa na uwezo wa kutibu maradhi haya.