Habari Mseto

Wakazi wa Msambweni wanaamua leo wanayetaka kuwawakilisha

December 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

FADHILI FREDRICK Na BENSON MATHEKA

BAADA ya vigogo wa kisiasa kukita kambi Msambweni kwa miezi miwili kupigia debe wagombeaji tofauti katika uchaguzi mdogo, wapigakura wa eneo hili leo watafanya uamuzi wa atakayewaakilisha bungeni hadi 2022.

Miongoni mwa wanasiasa wakuu waliofika eneo hilo kufanya kampeni ni kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na magavana Hassan Joho wa Mombasa na Jafferson Kingi wa Kilifi ambao waliongoza kampeni za Omar Boga wa chama hicho.

Gavana Salim Mvurya, aliyekuwa seneta wa Mombasa Omar Hassan na wanasiasa wanaomuunga Naibu Rais William Ruto nao walikuwa wakimpigia debe Faisel Beder, ambaye ni mgombea wa kujitegemea.

Kampeni za Msambweni ziliibua joto la kisiasa pande zote zikiuza sera zake lakini utulivu ulishuhudiwa katika eneobunge hilo lililo na wapigakura 69,003 ambao wanaelekea vituoni kuamua ni nani atakayekuwa mbunge.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori mnamo Machi.

Bw Boga na Bader wanashindana na Marere Wamwachai (National Vision Party), Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy), Khamis Mwakaonje (United Green Movement) na Shee Abdulrahman. Wagombea wengine wa kujitegemea ni Mansury Kumaka na Charles Bilali.

Kulingana na wenyeji ni vigumu kubashiri ni nani atakayekuwa mshindi kati ya Boga na Bader.

Lakini baadhi ya wakazi wanasema kuingiliwa kwa siasa za Kwale na viongozi wa kaunti ya Mombasa itawaponza sana.

Wakazi hao wanasema viongozi wa mashinani wa ODM wamepuuzwa na wenzao wa Mombasa.

Wakati huo huo, wagombeaji wao wanataraji ushindi katika ngome zao.

Bw Bader anatarajia kushinda katika wadi za Ukunda Kinondo ambapo aliishi na mjomba wake Dori.

Ukunda ina angalau wapiga kura 21,500 waliojiandikisha wakati Kinondo ina wapiga kura 11,014.

Bi Mwachai, Mwakaonje na Abdulrahman ngome yao ni Ramisi yenye wapiga kura 18,569.

Bw Boga anatoka wadi Gombato/ Bongwe ambayo ina wapiga kura 17,538 waliojiandikisha.

Alihudumu kama MCA wa wadi hiyo hadi Uchaguzi Mkuu wa 2017 alipowania kiti cha Msambweni dhidi ya Dori.

Wadi ya Gombato/Bongwe pia ni Ngome ya Kumaka na Mwakulonda.

Leo Jumanne pia kuna chaguzi zingine ndogo za udiwani ikiwa ni pamoja na Kahawa Wendani katika Kaunti ya Kiambu.

Zingine ni Kisumu Kaskazini, Wundanyi/Mbale (Taita Taveta), Gaturi (Murang’a), Lake View (Nakuru) na Dabaso (Kilifi).