• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
TAHARIRI: Tuanze leo kukabili ghasia uchaguzini

TAHARIRI: Tuanze leo kukabili ghasia uchaguzini

KITENGO CHA UHARIRI

FUJO zilizoshuhudiwa jana eneobunge la Msambweni wakati wa uchaguzi mdogo, ni aibu na zafaa kuchunguzwa na maafisa wa usalama, ili wahusika wachukuliwe hatua.

Vurugu hizo zilionekana kuwa muendelezo wa fujo zilizotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra, Kaunti ya Nairobi, ambapo wanasiasa walishambuliana hadharani bila ya kuona aibu.

Kwenye fujo za jana, malumbano yalishuhudiwa katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, hasa Mambweni kwenyewe, ambako wanasiasa wanaounga mkono mwaniaji wa chama cha ODM na wale wa Naibu Rais William Ruto wanaomuunga mgombea wa kujitegemea, walizozana, huku kila upande ukidai kuwepo njama za kuwahonga wapigakura.

Maeneo yaliyokuwa na joto la siasa zaidi ni katika shule za msingi za Mwaroni (Ukunda) na Jomo Kenyatta (Bomani).

Katika shule ya Jomo Kenyatta, vikundi viwili vilirushiana mawe na kusababisha kuvunjwa kwa vioo vya magari sawa na kulivyozuka ugomvi kati ya Seneta wa zamani wa Kakamega Dkt Boni Khalwale na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Makabiliano haya bila shaka yanaonekana kuchochewa na dhana iliyopo kwamba ushindi wa mtu anayepingana na yule wa ODM ni ushindi wa Dkt Ruto. Na kwamba kushindwa kwa anayeungwa na Naibu Rais kunaendeleza ubabe wa kinara wa ODM Raila Odinga.

Inafahamika kwamba Bw Feisal Bader ni mgombea wa kujitegemea lakini kutokana na kuungwa mkono na Dkt Ruto, chama cha ODM kimejitokeza juu chini kuhakikisha kinahifadhi kiti hicho kilichoshikiliwa na marehemu Suleiman Dori.

Ubabe huu wa kisiasa ni kati ya mambo ambayo harakati za kurekebisha Katiba kupitia BBI zinalenga kurekebisha. Hata hivyo, ni wazi kuwa jambo hili halitakomeshwa na sheria yoyote, iwapo wanaohusika katika ghasia za aina hii wataachwa bila kuchukuliwa hatua.

Kuongeza nyadhifa kwa wanasiasa watakaoshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu hakutazuia wawaniaji ubunge na MCA kuzozana na kusababisha uharibifu.

Maadamu uchaguzi utaendelea kuwa wa watu kuonyeshana nani mwenye ufuasi zaidi, Wakenya wataendelea kushuhudia visa vya aina hii, ambavyo ni aibu na mfano mbaya kwa wananchi, hasa watoto.

Kabla hatujafikiria kumaliza uhuni uchaguzini kupitia BBI, yafaa tuanze kuwatumia wazuaji fujo kwenye uchaguzi wa jana kama mfano kwa wengine.

You can share this post!

MWALIMU KIELELEZO: Millicent Achieng wa Shule ya Msingi ya...

WANGARI: Mzozo wa FKF, vyombo vya habari usuluhishwe upesi