GWIJI WA WIKI: Rose Okelo
Na CHRIS ADUNGO
KIZURI unachokifikiria ndicho utakachokipata.
Kipende kwa dhati hicho unachokifanya na namna unavyokifanya. Usifanye jambo kwa sababu wengine walilifanya au wanalifanya. Upekee wa mtu ndio ubora wake!
Mwalimu anayeyachangamkia majukumu yake na kulishabikia somo lake huwa kielelezo na mfano wa kuigwa miongoni mwa wanafunzi wake.
Marafiki wanaweza kukujenga au kukubomoa. Teua marafiki wema wenye fikira na uwezo wa kukutoa hapa na kukufikisha pale katika safari yako ya ufanisi. Fanya hivyo ili ufike mbali!
Mwanafunzi anayekubali kuongozwa na kuelekezwa ndiye hufaulu. Anastahili kufahamu uzito wa mzigo aliojitwika na awajibike kuubeba.
Mjenzi bora hujifunza ujenzi akaboreka hata zaidi. Mwandishi husoma kazi za watangulizi wake ndipo awe stadi na hodari kabisa. Huwezi kuwa mwalimu kabla ya kuwa mwanafunzi!
Huu ndio ushauri wa Bi Rose Katiba Okelo – mlezi wa vipaji, mwigizaji hodari na mwandishi wa vitabu ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya The Kenya High, Nairobi.
MAISHA YA AWALI
Rose alizaliwa mnamo 1968 katika eneo la Gwassi, Suba Kusini, Kaunti ya Homa Bay. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bi Christine Katiba na marehemu Bw Charles Katiba.
Mbali na Doreen Achia ambaye ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za injili, ndugu wengine wa Rose ni walimu kitaaluma. Hawa ni Mary Ojuka (Orero, Homa Bay), Deborah Onyango (Nyangubo, Kaunti ya Migori) na Richard Katiba (Kitawa, Homa Bay).
Rose alianza safari yake ya elimu mnamo 1974 katika Shule ya Msingi ya Shimo la Tewa, Mombasa. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya Kiabuya, Homa Bay alikosomea kwa mwaka mmoja (1975) kabla ya kurejea Shimo la Tewa kati ya 1976 na 1980.
Alifanya vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Coast Girls, Mombasa kati ya 1981 na 1984. Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCE), aliendeleza masomo ya kiwango cha ‘A-Level’ katika shule hiyo ya Coast Girls kati ya 1985 na 1986.
Rose alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kagumo, Kaunti ya Nyeri mnamo 1988 na akahitimu katika mwaka wa 1990. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza) kati ya 1995 na 1999.
Rose anatambua ukubwa wa mchango wa babaye mzazi katika kumlea kwa kumcha Mungu, kumhimiza masomoni, kumshajiisha maishani na kumwelekeza katika mkondo wa nidhamu kali. Miongoni mwa walimu waliomchochea kukichangamkia Kiswahili ni Bi Buko, Bi Ali na Bw Kachila waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Coast Girls.
Anakiri kwamba uamuzi wa kuzamia taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa mno na Bi Florence Mukuzi (marehemu) aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika Shule ya Msingi ya Shimo la Tewa.
UALIMU
Baada ya kukamilisha masomo ya A-Levels mnamo 1986, Rose alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Dzitsoni, eneo la Chonyi, Kaunti ya Kilifi.
Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Kahuhia Girls, Kaunti ya Murang’a kwa kipindi kifupi kabla ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumtuma katika Shule ya Upili ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale.
Alihudumu huko kati ya Mei 1990 na Mei 1991 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Luora, Homa Bay alikofundisha hadi Juni 1994 akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.
Rose alifundisha katika Shule ya Upili ya Upper Hill, Nairobi (Julai – Septemba 1994) kabla ya kuelekea Nairobi School (Septemba 1994 – Disemba 2018). Ilikuwa hadi Januari 2019 alipojiunga na Shule ya Upili ya The Kenya High.
Rose amekuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi ya Pili ya Kiswahili (102/2 Matumizi ya Lugha) tangu 1992. Uzoefu anaojivunia katika utahini umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kupigia chapuo Kiswahili, kuhamasisha walimu na kuwaelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne (KCSE).
Tangu 2004, amekuwa mwanajopo katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala ya Kenya (KICD) akishughulikia utayarishaji wa nyenzo za kufundishia.
Mbali na kushiriki vipindi vya uchambuzi wa vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya, Rose pia amekuwa katika mstari wa mbele kufyatua kanda za video kwa minajili ya mafunzo ya mitandaoni kupitia EDU TV Channel.
DRAMA
Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili katika shule zote ambazo amefundisha, Rose amekuwa akiwashirikisha wanafunzi wake katika mashindano mbalimbali ya kuigiza.
Aliwahi kuwa Mlezi wa Chama cha Drama cha Nairobi School (2007-2018) na akaongoza waliokuwa wanafunzi wake shuleni humo kutawazwa mabingwa wa kitaifa wa tamasha za drama mnamo 2008 wakiigiza mchezo wa Forty Minutes uliotungwa na Bw Nelson Ashitiva.
UANDISHI
Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Rose tangu alipojitosa katika ulingo wa ualimu. Kariha na ilhamu zaidi ya kuandika ilichochewa na waliokuwa wanafunzi wake Nairobi School.
Mbali na Bw Ben Wafula, mwingine aliyempigia Rose mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili ni Mkurugenzi wa One Planet Publishers, Bw Kithusi.
Rose alishirikiana na Bw Wafula kuandika kitabu KCSE Homestretch Udurusu na Mitihani ya Kiswahili kilichochapishwa na One Planet mnamo 2014.
Kwa sasa anaandaa miswada ya hadithi fupi za Kiswahili kwa matarajio kwamba kazi hizo zitachapishwa hivi karibuni. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuandika kazi za ushauri nasaha kwa Kiswahili.
JIVUNIO
Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Rose amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali nchini.
Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika hafla mbalimbali za makuzi ya Kiswahili.
Rose aliwahi kuchangia mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi ‘Kiswahili Kitukuzwe’ (2004-2010, KBC TV) na ‘Kamusi ya Changamka’ (2004-2005, QFM na QTV).
Kwa pamoja na mumewe Bw James Okelo, wamejaliwa watoto watano – Jan Okelo, 28, Sydney Katiba, 27, John Okelo (marehemu), Ben Ambrose, 20, na Beavan Okelo (marehemu). Rose anawastahi sana wajukuu wake – Jamal Kumu na Waridi Katiba.