Chebukati apuliza kipenga kuashiria kinyang'anyiro cha Matungu Machi 4, 2021
Na CHARLES WASONGA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Matungu utafanyika mnamo Machi 4, 2021.
Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati Jumatano alisema kila chama ambacho kinataka kushiriki katika uchaguzi huo mdogo na zingine za udiwani viwasilisha majina ya wagombeaji wao kabla ya Desemba 21, 2020.
Kwenye tangazo rasmi lililochapishwa katika gazeti rasmi la serikali Bw Chebukati pia alivitaka vyama kuwasilisha tarehe ambapo vitafanya mchujo kuteua watakaopeperusha bendera zao katika chaguzi hizo.
“IEBC itachapisha katika gazeti rasmi la serikali majina ya watu watakaoshiriki katika michujo ya vyama na tarehe ya shughuli hizo siku saba baada ya kupokelewa kwa majina ya wagombea hao,” Bw Chebukati akasema.
Mwenyekiti huyo vile vile alisema kuwa wagombea ambao wananuia kushiriki katika chaguzi ndogo kama wagombea wa kujitegemea hawapaswi kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa miezi mitatu kabla ya siku ya upigaji kura.
Isitoshe, Bw Chebukati alivitaka vyama vya kisiasa vinavyonuia kupeana tiketi za moja kwa moja kuwasilisha orodha ya watu hao walioteuliwa kabla ya Januari 4, 2021.
“Tarehe za uidhinishwaji wa wagombeaji walioteuliwa na vyama na wale wasiodhamini na vyama ni Januari 11, 2021, na Januari 12, 2021.
“Wagombeaji watahitajika kuwasilisha stakabadhi zao za uteuzi wa maafisa wasimamizi wa uchaguzi kati ya saa mbili asubuhi na saa saba mchana na kati ya saa nane mchana na saa kumi za jioni, katika afisin husika za IEBC,” Chebukati akaeleza.
Kiti cha ubunge cha Matungu kilisalia wazi kufuatia kifo cha Justus Murunga mnamo Novemba 15, 2020.
Chaguzi zingine ndogo za udiwani zitafanyika mnamo Januari 4 katika wadi za Huruma (Uasin Gishu), Hell’s Gate (Nakuru), London (Nakuru), Kiamokama (Kisii) na wadi ya Kitise/Kithuku (Makueni).