Habari Mseto

Korti yazuia magavana kufuta mawaziri kiholela

December 17th, 2020 2 min read

Na DERICK LUVEGA

MAGAVANA sasa hawatakuwa na mamlaka ya kuwafuta kazi kiholela makatibu, mawaziri wa serikali za kaunti na maafisa wakuu wa idara mbali mbali katika serikali hizo kabla ya miaka mitano.

Mahakama ya Leba inasema kwamba kandarasi zao zinafaa kuwa za miaka mitano, muhula ambao magavana huwa wanahudumu.

Kufuatia uamuzi huo katika kesi ambayo karani wa Kaunti ya Vihiga aliwasilisha kortini, maafisa hao wa serikali za kaunti watakuwa na muda mrefu wa kuhudumu isipokuwa wale wanaofutwa kwa sababu mbali mbali.

Jaji Stephen Radido wa Mahakama ya Leba mjini Kisumu, pia alizima magavana kuwawekea maafisa hao vipindi vya kuhudumu bila kushirikisha bodi za huduma za kaunti.

Uamuzi huo ni pigo kwa magavana ambao wamekuwa wakiwaajiri mawaziri wa serikali zao na maafisa wakuu kwa kandarasi za miaka mitatu au miwili.Baadhi ya magavana wamekuwa wakiwaajiri maafisa hao kwa muda mfupi wakidai wanataka kuona iwapo utendakazi wao ni wa kuridhisha.

Kesi hiyo imekuwa kortini kuanza Oktoba 2, 2019, wakati aliyekuwa karani wa Kaunti ya Vihiga Francis Ominde, aliposhtaki Gavana Wilbur Ottichillo kwa kumfuta kazi.

Gavana Ottichillo alitisha kupunguza kandarasi za Bw Ominde, mawaziri wake kuni na maafisa 11 wa idara za serikali yake. Bw Ominde aliwataja maafisa hao kama wahusika katika kesi aliyomshtaki Gavana Ottichillo, bunge la Kaunti ya Vihiga na serikali ya Kaunti hiyo.

Gavana Ottichillo alikuwa amewaajiri mawaziri wa serikali yake kwa kandarasi ya miaka miwili na kusema angeongeza muda huo kwa kutegemea utendakazi wa mtu binafsi. Kaunti nyingine zilikuwa zikiajiri maafisa hao kwa mfumo huo magavana wakisema nia yao ilikuwa ni kuimarisha utendakazi.

Kwa mfano, katika kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang aliwaagiza mawaziri wa serikali yake kutia saini barua za kuwafuta kazi zisokuwa na tarehe walipokuwa wakiapishwa Oktoba 24, 2017.

Alisema hii ingefanya kuwa rahisi kwake kuwafuta wakikosa kutimiza viwango alivyowawekea vya utendakazi.

“Hii ni thibitisho kwamba sitavumilia chochote kitakachohatarisha ajenda yangu ya mabadiliko kwa kuwa ni mimi nitakayelaumiwa na wapigakura. Ni lazima mfanye kazi kwa bidii,” Gavana Sang alisema wakati huo.

Msasa

Makarani wa kaunti, mawaziri na wakuu wa idara za kaunti huteuliwa na magavana. Hata hivyo, huwa wanahojiwa na kupigwa msasa vikali.

Jaji Radido alisema hatua hiyo sio ya kisheria na kuamua kwamba magavana hawana mamlaka ya kisheria ya kuweka muda wa kuhudumu wa maafisa wakuu wa serikali zao. Alisema kwamba kufanya hivyo kunahitaji mchango wa bodi za huduma za umma za kaunti ambazo kisheria, zina jukumu ya kuajiri wafanyakazi wa serikali za kaunti.

“Ni jukumu la bodi za huduma za umma za kaunti kuweka vipindi vya kuhudumu vya mawaziri wa serikali za kaunti, makarani wa kaunti na maafisa wakuu wa idara,” aliamua.

Aliongeza: “ Muda wa kuhudumu wa waziri wa serikali za kaunti unafungamana na kipindi cha kuhudumu cha gavana isipokuwa waondolewe ofisini kisheria,”