• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
KAMAU: Uchezaji kamari umekuwa ‘sumu’ kwa kizazi cha sasa

KAMAU: Uchezaji kamari umekuwa ‘sumu’ kwa kizazi cha sasa

Na WANDERI KAMAU

MIONGONI mwa mambo aliyosisitiza sana babu yangu kabla ya kifo chake ni kuhusu umuhimu wa kutia bidii kazini.

Babu alisema kuwa ni kupitia kwa bidii na kujitolea ambapo mwanadamu anaweza kufikia malengo yake maishani.

Kwenye vikao vingi vya hadithi alivyoshiriki na wajukuu wake kila jioni, babu pia alisisitiza kuwa: ‘Maisha si bahati nasibu.’

Mauko yalipomfika zaidi ya miaka 20 iliyopita, huo ndio ulikuwa ujumbe wake wa mwisho kwetu: “Daima kumbukeni kuwa lazima mfanye kazi ili mfanikiwe maishani. Njia zozote za mkato zitawaletea majuto baadaye.”

Narejelea usemi huo wa babu kutokana na hatua ya serikali kufutilia mbali leseni za baadhi ya kampuni za uchezaji kamari humu nchini.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alifichua jinsi alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya watu serikalini, alipowafurusha baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo.

Kwa mujibu wa Dkt Matiang’i, baadhi ya maafisa wakuu serikalini walipokea hongo kutoka kwa wakurugenzi hao ili kujaribu “kuwaokoa” dhidi ya mjeledi wa kurejeshwa makwao.

Je, ni vipi tungeweza kutetea mfumo ambao uliwageuza vijana kuwa mazuzu na watu wa kubahatisha maishani?

Mbali na Dkt Matiang’i, wakuu wa vyuo vikuu vile vile walieleza jinsi wanafunzi waliathiriwa vibaya, kwani wengi hawakuwa wakihudhuria masomo yao.

La kushtua ni kwamba, wachache ambao walihudhuria masomo walikuwa wakitumia muda mwingi kwenye simu zao wakijaribu “kubahatisha kufaulu maishani.”

Vijana

Bila shaka, ni dhahiri kwamba ongezeko la kampuni za uchezaji kamari nchini lilikuwa limesambaratisha na kuvuruga misingi ya maisha ya maelfu ya vijana.

Familia changa zilitekwa na wimbi la uchezaji kamari, kwani maelfu ya vijana walielekeza fedha chache ambazo walipata kwenye vibarua katika uraibu huo.

Talaka zikaongezeka, majuto yakakolea, nayo maafa yakaripotiwa kila kuchao katika sehemu mbalimbali nchini.

Mamia ya vijana waliripotiwa kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati ama kujitoa uhai, baada ya kushindwa “kupata mamilioni ya pesa” licha ya kutumia karibu mapato yao yote kwenye uraibu huo.

Ingawa wafanyabiashara wachache walitabasamu kwa kupata mamilioni kutokana na biashara hiyo, hatua hii iligeuka kuwa laana kuu kwa maelfu ya vijana na wanafunzi.

Wengi walisahau kauli ya babu kuhusu umuhimu wa kutia bidii maishani, na badala yake kutafuta njia za mkato kupata ufanisi.

Kwanza, lazima serikali iweke sera kali kudhibiti uchezaji kamari nchini, hata miongoni mwa kampuni chache ambazo bado zinaendelea kuhudumu.

Utakuwa mkasa kwetu na kizazi cha sasa ikiwa jamii itaendelea kutazama maovu haya yakiendelea bila kuyakemea.

Ingawa harakati za kurejesha urazini katika sekta hiyo zimeanza, tusikubali tena uozo huo kuvuruga misingi ya maadili yetu.

Ni lazima tuendelee kukisisitizia kizazi cha sasa kuhusu umuhimu wa kutia bidii maishani na kujivunia jasho la juhudi zao, badala ya kutumia njia za mikato.

Hatua hii itapalilia moyo wa bidii.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Ni mapema mno kututwika mzigo

TANZIA: Gavana John Nyagarama afariki jijini Nairobi