TANZIA: Gavana John Nyagarama afariki jijini Nairobi
Na RUTH MBULA
GAVANA wa Kaunti ya Nyamira John Obiero Nyagarama amefariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 74 katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akitibiwa kwa muda wa mwezi mmoja.
Duru zinasema Nyagarama alikuwa na matatizo ya kiafya yatokanayo na ugonjwa wa Covid-19.
Familia yake imeambia Taifa Leo kwamba alikuwa anatatizika kupumua baada ya mapafu kushindwa kufanya kazi.
Wakati wa uhai wake amekuwa akiwahamasisha wakazi wa Nyamira kuhusu umuhimu wa kuzingatia masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya kuzuia kuenea kwa Covid-19.
Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo aliugua Covid-19 mwanzoni mwa Novemba akatibiwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi kwa kipindi cha wiki tatu.
Mke wa kwanza wa Nyagarama, Bi Dorcas Sigara, alifariki 1998, akimuacha na watoto 10 lakini kijana wake mkubwa George Ndemo Nyagarama, alifariki Juni 11, 2018, baada ya kuugua kwa muda.
Nyagarama baadaye alimuoa mke mwingine kwa jina Naomi. Watoto wake wengine ni Emily, Kefah, Gideon, Mary, Erick, Isaiah, Sam, Tom na marehemu Catherine.