Madarasa zaidi kujengwa Ruiru kwa kiasi cha Sh7 milioni
Na LAWRENCE ONGARO
KUNA haja ya kufanya matayarisho ya mapema ya mabadiliko hasa shule za msingi.
Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara ametenga Sh7 milioni kuona ya kwamba eneo la ekari tatu kunajengwa shule katika kijiji cha Gatong’ora na Mutonya.
Alisema katika shule ya msingi ya Mwiki iliyoko eneo la Githurai, kuna wanafunzi wapatao 4,000 idadi aliyosema ni hatari katika wakati huu wa janga la Covid-19.
“Ni wazi ya kwamba wanafunzi hao wote kwa sasa hawawezi kukubaliwa kujumuika pamoja. Kwa hivyo, nimetenga fedha za NG-CDF za maendeleo ya eneobunge la Ruiru ili kupunguza wanafunzi wengine kupelekwa katika madarasa mapya yatakayojengwa Gatong’ora na Mutonya,” alisema Bw King’ara.
Alieleza ya kwamba tayari mradi huo umezinduliwa na inatarajiwa utakamilika baada ya miezi miwili hivi.
“Tunataka mwaka ujao wa 2021, wanafunzi wasisongamane katika madarasa. Hii ndiyo maana tunaharakisha mpango huo,” alisema Bw King’ara.
Alisema cha muhimu kwa wakati huu ni kuhakikisha shule za msingi zinawekeza katika uhifadhi wa maji kwa wingi na vyoo vya kutosha.
“Ninaelewa ya kwamba walimu watakuwa na changamoto kubwa ya kukabiliana na kuhamasisha wanafunzi jinsi ya kudumisha usafi kila mara. Kwa hivyo, kuanzia Januari 4, 2020,wazazi wana jukumu la kuwapeleka wana wao shuleni ili waendelee na masomo baada ya mwaka mmoja nje,” alisema mbunge huyo.
Aliwashauri wazazi wawe makini hasa wakati huu wa likizo kwa kuona ya kwamba wanafuatilia marafiki wanaojumuika na wana wao.