Wawili wanusurika kifo Thika Road baada ya gari walimokuwa kubingiria likikwepa basi lililoegeshwa kukarabatiwa
Na SAMMY WAWERU
WATU wawili wamenusurika kifo baada ya gari walimokuwa kuhusika katika ajali katika barabara Thika Superhighway mapema Ijumaa.
Ajali hiyo iliyotokea eneo la Carwash, kati ya Roysambu na Githurai, ilihusisha magari mengine mawili.
Kulingana na walioshuhudia, gari aina ya Subaru lenye nambari za usajili KBV 665Y na lililokuwa na manusura lilibingiria wakati likijaribu kuhepa basi lililosimama kwa minajili ya ukarabati.
Basi hilo ni la kampuni moja inayohudumu kati ya mtaa wa Githurai na jiji la Nairobi.
“Lilikuwa kwa mwendo wa kasi katika leni ya kasi, likijaribu kuhepa lori lililokuwa likiundwa likakwaruza gari lingine na kubingiria. Ni kwa neema ya Mungu waliokuwa ndani wamenusuruika,” akaelezea mmoja wa walioshuhudia, na ambaye ni mhudumu wa bodaboda.
Ni mkasa uliosababisha msongamano wa magari kati ya Roysambu na Githurai kwa muda wa saa moja nusu.
“Tunaendelea kuhimiza madereva wawe waangalifu barabarani hasa tunapoelekea msimu wa Krismasi. Mwendo wa kasi ni hatari na unaua,” akasema afisa mmoja wa trafiki aliyefika eneo la ajali, akiwataka madereva kuwa makini na waadilifu.
Thika Road, eneo la Carwash leni ya kasi imekuwa ikishuhudia mikasa ya mara kwa mara ya ajali.
Uendeshaji magari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha leni bila uangalifu, umetajwa kama kiini cha ajali nyingi Thika Superhighway.