Sonko aliiga Trump kuongoza
Na WANDERI KAMAU
KWA muda aliohudumu akiwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi kati ya 2017 na Alhamisi, Bw Mike Sonko alimuiga Rais wa Amerika Donald Trump kwenye mbinu za uongozi wake.
Kama Rais Trump, Bw Sonko alikuwa na mazoea ya kuwahangaisha maafisa wakuu kwenye serikali yake kwa kuwahamisha kutoka wizara moja hadi nyingine wakati wowote aliotaka na kuwafuta wengine.
Hadi kung’atuliwa mamlakani na Seneti hapo Alhamisi, Bw Sonko alikuwa amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri zaidi ya mara sita.
Miongoni mwa mawaziri waliojipata kwenye patashika hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Elimu Muthoni Ouko, aliyekuwa Waziri wa Fedha Charles Kerich, Bi Vesca Kangogo (Mazingira) kati ya wengine.
Kabla ya kufutwa kazi na Bw Sonko Septemba mwaka uliopita, Bw Kerich ndiye alikuwa waziri aliyezungushwa sana katika wizara. Kwanza, aliteuliwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kabla ya kuhamishiwa katika Wizara ya Ardhi, baada ya mtangulizi wake, Bw Peter Njuguna kufutwa kazi na Bw Sonko.
Baadaye, aliteuliwa kuhudumu katika Wizara ya Fedha mnamo Aprili mwaka huo huo, baada ya Bw Sonko kumfuta kazi Bw Danvas Makori.
Kama hilo halikutosha, Bw Sonko alimhamishia Bw Kerich katika Wizara ya Afya baada ya kumfuta kazi Bi Kangogo.
Mnamo Julai mwaka uliopita, Bw Sonko alimteua Bw Kerich kama “Mkubwa wa Mawaziri” kwa kumpa jukumu la kusimamia wizara zote. Hata hivyo, alimfuta kazi Septemba 25, 2019.
Bw Sonko pia alikuwa na mazoea ya kuviingilia vyombo vya habari ama kuwatukana wanahabari kila mara alipohisi vimemwingilia.
Rais Trump naye amekuwa na mazoea ya kuviingilia vyombo vya habari akisema vimekuwa vikimharibia sifa.