Michezo

Neymar kurejea uwanjani kusakatia PSG mnamo Januari 2021 baada ya kupona jeraha

December 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

FOWADI matata wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr anatarajiwa kurejea uwanjani kusakata soka mnamo Januari 2021 baada ya kupona jeraha alilolipata wakati akichezea kikosi chake dhidi ya Olympique Lyon mnamo Disemba 13, 2020.

Neymar, 28, alionekana akijigaragaza chini kwa maumivu makali na akalazimika kuondolewa uwanjani kwa machela baada ya kuchezewa visivyo na Thiago Mendes aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika mechi hiyo.

“Kuna jeraha alilolipata kwenye mfupa na anaendelea kupata matibabu. Anatarajiwa kurudi Januari,” ikasema sehemu ya taarifa ya PSG.

Kocha mkuu wa PSG, Thomas Tuchel alikuwa amedokeza awali kuhusu uwezekano wa Neymar kuwajibishwa dhidi ya Lille katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Disemba 20, 2020.

Kwa mujibu wa taarifa ya PSG, Neymar atakuwa amepona kabisa kiasi cha kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa dhidi ya Barcelona kwenye mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari.

Neymar alijiunga na PSG kutoka Barcelona kwa kima cha Sh26 bilioni mnamo Agosti 2017.

Mbali na kusaidia PSG kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligue 1, Neymar aliwezesha waajiri wake kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 ila wakazidiwa maarifa na Bayern Munich kutoka Ujerumani.