• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Sonko alaumu mkono wa Raila, Uhuru kwa masaibu yake

Sonko alaumu mkono wa Raila, Uhuru kwa masaibu yake

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko, ameanza kutapatapa kuhusu masaibu yake ya kisiasa akiwalaumu viongozi wa vyama vya kisiasa kwa kushinikiza maseneta kuidhinisha kuondolewa kwake mamlakani.

Bw Sonko alisema maseneta walipigiwa simu na viongozi wa vyama vyao kuwaagiza kupiga kura kumuondoa afisini kwenye kikao spesheli kilichoandaliwa Alhamisi.

Bila kutoa ushahidi, Bw Sonko alidai kila seneta alipokea simu kutoka kwa kiongozi wa chama chake kumuagiza aunge hatua ya bunge la kaunti ya Nairobi ya kumvua mamlaka yake.

Maseneta wanane walikataa kuidhinisha kuondolewa kwake na wawili wakataa kupiga kura. Alijikanganya kwa kudai kwamba, maseneta walipatiwa Sh2 milioni kila mmoja na serikali ili kuunga mswada huo.

Kulingana na Seneta huyo wa zamani wa Kaunti ya Nairobi, maseneta walipatiwa pesa hizo na serikali kama zawadi ya Krisimasi ili wakubali kumfurusha.

“Wakati wa kupiga kura, serikali iliwapa maseneta Sh2 milioni kama zawadi ya Krisimasi ili wakiuke sheria,” Bw Sonko alisema kwenye taarifa kupitia mitandao ya kijamii bila ithibati yoyote.

Bw Sonko ambaye alihudumu kama seneta wa kaunti ya Nairobi kabla ya kuchaguliwa gavana 2017, alidai kuwa maseneta hawakumuondoa kwa hiari yao.

“Ilibidi baadhi ya waliokuwa wenzangu katika seneti kunisulubisha kwa sababu ya shinikizo za kisiasa kutoka kwa wakuu wa vyama vyao waliopigia simu kila mmoja kuwaagiza wanitimue kwa sababu mimi sikuzaliwa Ikulu na baba yangu hakuwa rais, waziri mkuu au makamu wa rais,” Bw Sonko alidai bila kutaja mashtaka yaliyomkabili katika seneti.

Wachanganuzi wanasema kwamba Sonko hafai kulaumu maseneta kwa masaibu yake.

“Hawezi kulaumu maseneta kwa kuwa hawakuanzisha mchakato wa kumtimua. Angezima juhudi za kumtimua katika bunge la Kaunti lakini hakufaulu. Jukumu la seneti ni kuchunguza shughuli za kaunti na kuidhinisha hatua zinazochukua kwa kura na ndivyo maseneta walifanya kwa Sonko,” asema mchanganuzi wa siasa wakili Thomas Maosa.

Anasema kucheleweshwa kuapishwa kwa spika wa bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura kuwa kaimu spika hakuwezi kumpa Sonko nafasi ya kupinga uamuzi wa seneti.

“Hakuna mwanya wa kukataa rufaa dhidi ya uamuzi wa seneti. Kuchapishwa ilani ya kutimuliwa kwake kuliweka kikomo mchakato huo,” alisema.

Bw Sonko alionekana kusalinu amri kwa kusema mkasa mkubwa kwa mwanadamu sio kuangushwa bali ni kukataa kuamka baada ya kubwagwa.

Bw Mutura angeapishwa kuhudumu kama kaimu spika Ijumaa lakini shughuli hiyo ikaahirishwa jaji alipofika akiwa amechelewa. Licha ya masaibu yake aliwafariji wafuasi wake akiahidi kuendelea kuwasaidia.

“Kwa wote waliosimama nami katika miaka yangu 10 katika siasa, hata mambo yakiwa magumu vipi, msife moyo, licha ya yaliyotendeka au yatakayonipata, nitasimama nanyi na nitaendelea kuwasaidia,” alisema.

You can share this post!

Tovuti ya IEBC yakwama watu wakiomba kazi

JAMVI: Jinsi ilivyo ni siasa za 2022 zitaamua mrithi wa...