'Ukiwa na mipango maalumu si ajabu ufugaji wa kuku ukuingize kwenye ligi ya wakwasi'
Na SAMMY WAWERU
WATAALAMU wa ufugaji wanasema mchango wa kodi ya ushuru kutoka sekta ya ufugaji wa kuku unaweza kuongezeka ikiwa wakulima watatilia maanani shughuli za ufugaji.
Kikwazo kilichopo hata hivyo ni kuwepo kwa soko duni la mazao ya kuku, yaani nyama na mayai. Soko la mayai ndilo limeathirika kwa kiasi kikubwa.
Mahangaiko hayo yanatokana na mikakati duni ya serikali kuimarisha ufugaji wa kuku nchini. Mosi, gharama ya ufugaji wa ndege hawa wa nyumbani ni ya juu mno, hasa kutokana na kuendelea kukwea kwa bei ya chakula cha kuku.
“Malighafi kutengeneza lishe ya mifugo ni ghali mno, na ndio maana chakula kinazidi kuwa ghali,” anasema Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya mifugo hususan ufugaji wa kuku.
Ughali wa malighafi, ndio chocheo la watengenezaji wa lishe ya mifugo kuongeza bei. Ni kizingiti kinachozima ari ya wakulima wengi kuendeleza ufugaji wa kuku.
Isitoshe, wafugaji limbukizi wakikokotoa hesabu, kwa kulinganisha gharama ya kufuga kuku na mapato, wanakufa moyo.
Baadhi ya vyakula havijaafikia ubora wa bidhaa, na vinaendelea kusambazwa sokoni, hii ikiwa na maana kuwa mfugaji atakinunua au kuvinunua ila ufugaji wake hautaimarika wala kustawi, kwa kuwa kuku hawapati lishe yenye virutubisho faafu.
Kando na matibabu, usafi wa hali ya juu kwenye vizimba, chakula chenye virutubisho na madini faafu na ya kutosha, ndio msingi wa mazao bora ya mayai na kuku.
“Kabla nianze kujitengenezea chakula cha kuku, nilikuwa nakadiria hasara chungu nzima kutokana na lishe ambayo haijaafikia ubora wa bidhaa,” anaelezea Hesbon Asava, mfugaji.
Hesbon, 67, anasema alianza ufugaji wa kuku mwaka wa 1992 na kufikia mwaka wa 2013, mambo yalikuwa yamebadilika kwa kile anataja kama “kusheheni kwa chakula duni cha kuku, ambacho hakijaafikia ubora”.
Anaeleza kwamba awali alikuwa akifuga zaidi ya kuku 500.
Mtaalamu Ngura anahimiza wakulima kukumbatia uundaji wa chakula, ili kuepuka vikwazo hivyo.
“Walioweza kufanikisha ufugaji wa kuku ni wanaojitengenezea lishe, kwa kutumia malighafi yaliyopo nchini,” mdau huyo anafafanua, akisema hatua hiyo mbali na kuwa na uhakika wa lishe bora, inapunguza gharama.
Punje za mahindi, ngano, maharagwe aina ya soya, samaki wadogo aina ya Omena na laimu ni kati ya malighafi yanayotumika kutengeneza chakula cha kuku.
Kuku pia hulishwa majani ya mboga kama vile sukuma wiki, spinachi na pia kabichi, ili kuinua kiwango chao cha Vitamini.
Kulingana na mtaalamu Okuta Ngura, kinachoangusha wakulima wengi ni kutokuwa na mipangilio maalumu. “Ukikosa kupanga mikakati yako unapoingilia ufugaji wa kuku, basi unapanga kufeli,” anaonya.
Ngura anasema kufanikisha ufugaji wa kuku si jambo gumu. “Mipango mahususi itakuvunia faida,” anahimiza.
Mtaalamu huyo anasema mwanzo mfugaji aweke paruwanja nia yake kufuga kuku, ikiwa anataka wa nyama au wa mayai.
“Kuku wa nyama hukomaa miezi sita baada ya kuanguliwa vifaranga, hivyo basi unapaswa kuwa na mpango wa miezi sita mfululizo, kuanzia matibabu, chakula na gharama nyinginezo,” Ngura anaelezea.
Pia, kuku huanza kutaga mayai baada ya miezi minne kuanguliwa.
Ngura anashauri mfugaji ahakikishe ana vizimba bora kabla kuingilia ufugaji wa kuku. Anapendekeza fundi azingatie kigezo cha futi moja kwa moja mraba, nafasi ya kila kuku ili kumruhusu ‘kucheza’.
“Gharama huwa utangulizi, hasa wakati wa utengenezaji wa vizimba. Mwaka wa pili, mfugaji anayezingatia vigezo faafu na kuwa na mipango murwa, ataanza kufurahia matunda ya jitihada zake,” anasema.
Mfugaji anakumbushwa kuhakikisha anazingatia chanjo, matibabu, hadhi ya juu ya usafi na kunywesha kuku wake maji safi na ya kutosha.
“Ninaamini hakuna jambo gumu ukijitolea. Kuku wanaweza kukuajiri na wakuingize kwenye ligi ya ukwasi,” anasema mtaalamu Ngura, na ambaye pia ni mfugaji wa kuku.