Habari Mseto

Miguna amezea ugavana Nairobi licha ya visiki

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA WANGU KANURI

WAKILI mbishi aliyenyimwa kibali cha kuingia nchini Kenya, Dkt Miguna Miguna, ametangaza kuwa atawania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Nairobi katika uchaguzi mdogo ujao baada ya Mike Sonko kutimuliwa na Seneti. Wakili huyo alichapisha hayo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

“Baada ya kupokea ushauri  wa kina wa kisheria kutoka kwake @waikwawanyoike Desemba 19, 2020, mimi Miguna Miguna, Mkenya wa kuzaliwa na mpigakura aliyesajiliwa katika Kaunti ya Nairobi, ninatangaza uwaniaji wangu wa gavana wa Nairobi katika uchaguzi mdogo ujao. Watakaojitolea kunisaidia wamekaribishwa,” aliandika.

Lakini mwanasheria huyo anaishi jijini Toronto, Canada ambapo ana uraia wa mataifa mawili, huku Wakenya wakishangaa iwapo atakubaliwa kuwania ugavana na Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC).

Mapema mwaka huu, Mkenya aliye na uraia wa Amerika Mwende Mwinzi alikumbana na changamoto katika azma yake kuwa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini kutokana na uraia wake wa mataifa mawili.

Juhudi za Dkt Miguna za kurejea nchini Kenya baada ya kufurushwa zimegonga mwamba huku ikiwa kama kinyang’anyiro cha mwenye nguvu mpishe kati yake na serikali.

Hata ingawa hajaweza kurejea nchini, maswali ya jinsi atakavyofanya kampeni za kuwania kiti hicho cha ugavana zinavitinga vichwa vya wakenya wengi huku wakiwa na hamu ya kujua kitakachoendelea.

Hali kadhalika tangazo lake limeibua hisia tata katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Je, hamfahamu kuwa ina maana gani iwapo atajileta nyumbani kwanza? Ama ataongoza Nairobi akiwa mbali kama kifaa cha Bluetooth?” akauliza @GodlovesRandom.

“Unastahili kuwa gavana wa Nairobi lakini hujasajiliwa kama mpigakura wa Nairobi na hilo litafanya uondolewe kwenye kinyanganyiro,” akasema EkaiLokaale.

“Una kura yangu kila wakati utakapowania nafasi yoyote nchini Kenya. Itakuwa furaha yangu kuchagua uongozi murua ulio na maono. Asante kwa nafasi nyingine ya kuthibitisha usaidizi wangu. Siwezi ngoja kupiga kura,” akaeleza @brunoclifford.

“Wakazi wa Nairobi hii ni nafasi yetu ya kuonyesha kuwa mamlaka yana watu. Tafadhali tumpigie kura Miguna kama gavana,” akasema @kennedymulinge.

“Miguna hatawasilisha kazi ipasavyo, atawanyanyasa masekretari watakaofanya kazi katika ofisi yake. Alifanya kazi katika ofisi ya Raila na wengi walipata ugonjwa wa shinikizo la damu! Miguna Miguna ni mwenye matusi mengi na asiye mstaarabu,” akaandika @zepphimobby78.

“Ninafikiri kabila si kikwazo kikuu katika kinyang’anyiro cha kiti cha ugavana cha Nairobi. Pesa hali kadhalika kwani unaweza toa hongo na upate njia ya kuwa gavana,” akaeleza @KarimWaiyaki.

“Ninaidhinisha @MigunaMiguna katika kinyang’anyiro kijacho cha kiti cha ugavana cha kaunti ya Nairobi. Wakati umewadia wa kusimama na uongozi wa kweli na si uongozi wa wastani kisa ushirika wa chama. Ninakuunga mkono Miguna Miguna,” akaandika @MillicentOmanga.