• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Wahudumu wa matatu washauriwa walipishe nauli ifaayo bila kudhulumu wasafiri

Wahudumu wa matatu washauriwa walipishe nauli ifaayo bila kudhulumu wasafiri

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa matatu wameshauriwa kufuata sheria za Covid-19 hasa wakati huu wasafiri wanaabiri magari kujumuika na familia zao wakati wa sherehe za sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike, amewahimiza wawe na utu kwa kulipisha nauli ilio nafuu.

“Huu sio wakati wa kujitajirisha haraka lakini ni vyema kujali wasafiri popote walipo. Wananchi wengi wamelemewa na mizigo mizito ya kimaisha,” alisema Bw Wanyoike.

Alisema usafiri itakuwa na msongamano wakati huu wa sikukuu kwa sababu kuna wanafunzi wa kidato cha nne,darasa la nane na la nne watakuwa pia wakirejea likizoni.

Alipendekeza Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA) na polisi wa trafiki waje pamoja na kufanya msako ili kunasa matatu zinazokiuka sheria za trafiki.

“Tunaelewa vyema wahudumu wa matatu watakuwa na tamaa ya kupata pesa maradufu kwa sababu ni msimu wa sherehe. Pia wanaendesha biashara hiyo huku wengi wao wakikosa kurekebisha magari yao kabla ya kusafiri mwendo mrefu,” akasema.

Kwa upande wa wasafiri aliwahimiza wawe na nidhamu kwa kuvalia barakoa, kunawa mikono na kuweka nafasi ya angalau umbali wa mita moja na nusu kutoka kwa mmoja hadi mwingine ili kukabiliana na Covid-19.

“Wananchi wengi wanaleta mzaha kwa kukosa kuvalia barakoa. Usivalie barakoa kwa sababu umeona polisi mbele yako, lakini fanya hivyo kwa manufaa yako mwenyewe na familia yako,” alisema Bw Wanyoike.

Alitoa wito kwa kila mwananchi kuwa na nidhamu na kuchunga maisha yake.

Kuhusu wafanyabiashara wa maduka, aliwaomba wauze bidhaa zao kwa bei nafuu.

“Hakuna haja ya kuuza bidhaa zenu kwa bei ya juu kupitia kiasi kwa sababu mwananchi wa kawaida kwa sasa hana chochote,” alisema Bw Wanyoike.

Aliwataka wanaosafiri mashambani ni wasitangamane kiholela wanaposherehekea.

“Jambo muhimu kwa wakati huu ni kujumuika kwa vikundi vichache ili kufuata kanuni za kiafya za kuzuia kuenea kwa Covid-19,” alifafanua kinara huyo.

You can share this post!

TIM WANYONYI SUPER CUP: Leads United yamaliza ubishi kwa...

Starehe Foundation FC yatwaa kombe la NG-CDF Thika