MakalaSiasa

WANDERI KAMAU: Ulaya irejeshe mali ya Afrika ambayo inamiliki kiharamu

December 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

TANGAZO la Rais Felix Tshisekedi wa DRC Kongo kwamba taifa hilo litachukua mabaki ya mwili wa mwanasiasa Patrice Lumumba kutoka Ubelgiji, limeashiria kuwa wakoloni bado wanaendelea kushikilia raslimali muhimu za Afrika.

Kwenye tangazo lake, Rais Tshisekedi alisema hatua hiyo inalenga kumpa marehemu Lumumba mazishi ya hadhi, kama mojawapo ya viongozi waliotoa mchango mkubwa sana katika ukombozi wa kisiasa wa taifa hilo kutoka kwa wakoloni.

Lumumba aliuawa kikatili mnamo Januari 1961, akiwa na miaka 35 pekee, kwenye njama inayodaiwa kuendeshwa kisiri na Ubelgiji kwa ushirikiano na Amerika.

Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.Bila shaka, kauli ya Rais Tshisekedi iliibua ukweli ambao umefichika kwa muda mrefu, kuhusu mali ya nchi za Afrika ambayo bado inaendelea kumilikiwa na mataifa ya Ulaya ambayo yalizitawala mwanzoni.

Hapa nchini, mwandishi na mwanahistoria Maina wa Kinyatti ameeleza mara kadhaa kuwa Uingereza bado inaendelea kushikilia stakabadhi muhimu zinazorejelea historia ya vita vya Mau Mau na vifo vya baadhi ya viongozi wake katika miaka ya hamsini.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio miaka kadhaa iliyopita, Prof Kinyatti alirejelea masaibu aliyopitia kwenye safari ya kuandika kitabu ‘Kimathi Letters’ (Barua za Kimathi).

Kitabu hicho kililenga kukusanya barua zote ambazo mpiganiaji uhuru Dedan Kimathi alikuwa akiwaandikia wapiganaji wa Mau Mau, kwani yeye alikuwa amesoma hadi kuwa mwalimu.

Prof Kinyatti alisema alishangaa sana alipogundua kuwa baadhi ya barua za shujaa huyo zinaendelea kushikiliwa na serikali ya Uingereza, ambapo ilikuwa vigumu sana kwake kuzipata.Zaidi ya hayo, alisema kwenye utafiti wake, alibaini kuna vifaa vingine muhimu vinavyorejelea historia ya Kenya ambavyo vimehifadhiwa katika makavazi kuu ya Uingereza, jijini London, badala ya kuwepo humu.

Kwa fichuzi hizo mbili kati ya zingine, ni wazi kuwa kuna mengi ambayo yamefichika kuhusu raslimali muhimu za Afrika zinazoshikiliwa na wakoloni wake hadi sasa.

Wakati nchi zilipojinyakulia uhuru wake katika miaka ya hamsini na sitini, lengo kuu lilikuwa kukata mahusiano yote ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii na mataifa hayo. Hilo ndilo lilikuwa maana kuu ya uhuru huo.Hata hivyo, inasikitisha kuwa kwa undani, maana halisi ya ‘uhuru’ ilikuwa kinyume na ilivyokusudiwa.

Hadi sasa, mataifa mengi yanaendelea kuwa watumwa wa wakoloni wao kwa karibu nusu karne sasa tangu kupata uhuru wao.Hilo limedhihirishwa na harakati za kutafuta chanjo dhidi ya virusi vya corona, kwani mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakizitazama nchi za Ulaya kupata chanjo hiyo.

Nchi hizo pia zimeiga wakoloni wake katika uendeshaji wa mifumo muhimu kama elimu, siasa, sayansi na hata tamaduni zake.Ili uhuru wa Afrika kupata maana kamili kama ilivyokusudiwa, lazima mataifa ya Ulaya yarejeshe mali yote ya nchi hizo inayomiliki.

[email protected]