• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
BBI si ya kutafutia ‘viongozi fulani’ vyeo serikalini – Kingi

BBI si ya kutafutia ‘viongozi fulani’ vyeo serikalini – Kingi

Na MAUREEN ONGALA

GAVANA Amason Kingi wa Kilifi, amewalaumu viongozi ambao wanaeneza uvumi kwamba mapendekezo yaliyo katika ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), yanalenga kubuni nyadhifa kwa baadhi ya wanasiasa nchini.

Hilo linajiri huku mbunge Aisha Jumwa wa Malindi akiendeleza kampeni dhidi ya ripoti hiyo, akiwarai wenyeji kuikataa kwani haizingatii matakwa yao.

Akihutubu mjini Kilifi, Bw Kingi alisema kuwa mapendekezo hayo yanalenga kuwafaidi Wakenya bila ubaguzi wowote.Hivyo, aliwaomba viongozi ambao wameisoma ripoti kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala inayoangazia badala ya kuwapotosha.

“Ikiwa wewe ni kiongozi na umesoma na kuielewa ripoti hiyo, waeleze wananchi ukweli bila kuwadanganya,” akasema.Bw Kingi pia aliwalaumu viongozi wanaoipinga ripoti, akisema wao ndio maadui wa wananchi kwani mapendekezo hayo yanalenga kuimarisha maendeleo ili kuwafaidi.

“Baadhi ya kaunti ni kubwa na zina mahitaji mengi sana. Hata hivyo, mgao wa asilimia 15 pekee ya mapato kutoka serikali ya kitaifa hauwezi kutosheleza mahitaji hayo. Hiyo ndiyo sababu kuu tunahitaji fedha nyingi kwenye kaunti,” akasema.

Aliwarai wananchi kupuuza viongozi wanaoipinga ripoti hiyo na badala yake kujisomea wenyewe.“Baadhi yetu hatujaisoma ripoti, lakini tunasema ni mbaya na haifai kwa Wakenya,” akasema.

Alieleza ameridhishwa na mabadiliko ambayo yalifanywa, kwani yataiwezesha kaunti hiyo kupata maeneobunge manne zaidi.Bi Juliet Riziki, maarufu kama ‘Kachachawa,’ ambaye ni mwanasiasa katika eneo hilo, alisema ripoti itawahamasisha wanasiasa, hasa madiwani kurudi shuleni kuongeza masomo.

“BBI itaimarisha kiwango cha masomo miongoni mwa viongozi katika maeneo ya mashinani,” akasema.Bi Riziki alisifu hatua ya kuhamisha nafasi ya wabunge wanawake kutoka Bunge la Kitaifa hadi Seneti, akisema hilo litawafanya kuwajibika zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mwanasiasa huyo aliwania nafasi ya mbunge mwanamke wa kaunti kama mwaniaji huru mnamo 2017, baada ya kushindwa kwenye zoezi la uteuzi katika chama cha ODM na Bi Getrude Mbeyu.

Alisema wanawake watashinikiza kupewa hazina maalum watakapoanza kuhudumu katika Seneti.Kauli hizo zinajiri huku baadhi ya wenyeji katika kaunti wakieleza kutoridhishwa na ripoti, wakisema inalenga kuwafaidi watu wachache nchini.

You can share this post!

Hofu ya maafa mgomo ukichacha

Gavana ataka wachochezi waanikwe