• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Oparanya asema atamuunga naibu wake kumrithi 2022

Oparanya asema atamuunga naibu wake kumrithi 2022

Na Shaban Makokha

GAVANA Wycliffe Oparanya wa Kakamega ametangaza kwamba atamuunga mkono naibu wake, Prof Philip Kutima, kurithi kiti hicho atakapoondoka uongozini 2022.

Ni tangazo linalotarajiwa kuzua mdahalo mkali wa kisiasa katika kaunti hiyo, kwani kwa muda mrefu Bw Oparanya hajasema lolote kuhusu nani atamrithi.

Wadadisi wa siasa za eneo hilo wanasema kuna uwezekano Bw Oparanya anampendelea Prof Kutima kwani ameonyesha uzalendo mkubwa kwake.Vile vile, amesifiwa pakubwa kutokana na uwezo wake kusimamia na kuendesha mipango ya serikali ya kaunti hiyo.

“Nimeteua Prof Kutima kwani ninafahamu utendakazi wake,nilipomteua mara ya kwanza kama naibu wangu wakati wa kampeni. Tulibuni ushirikiano mzuri sana. Mnamo 2017, nilimteua tena kwani ninafahamu utendakazi wake,” akasema Bw Oparanya.

Tangazo hilo linatarajiwa kuzua mielekeo tofauti kisiasa, hasa miongoni mwa wawaniaji waliotarajia atawaunga mkono kuwania nafasi hiyo ifikapo 2022.

Baadhi ya wale ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kusimamia Usambazaji wa Umeme (Ketraco) Fernandes Barasa, aliyekuwa Seneta wa kaunti hiyo Dkt Boni Khalwale, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Metropol Sam Omukoko, Seneta Cleophas Malala kati ya wengine.

You can share this post!

Wanasiasa wakosa adabu mazikoni

Uhuru awaruka Wakenya kuhusu ushuru nafuu