• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Demu ararulia polo long’i akisaka hela

Demu ararulia polo long’i akisaka hela

Na JOHN MUSYOKI

KOSOVO, MACHAKOS

KIZAAZAA kilizuka katika kilabu kimoja sehemu hii kidosho alipoangushiwa makofi na wateja kwa kurarua mfuko wa suruali ya jamaa akitaka pesa za kununua dozi.

Duru zinasema jamaa alikuwa ameahidi kumnunulia demu pombe siku moja lakini akadinda kutimiza ahadi yake.

Siku ya kioja, polo alipoenda kilabuni kupata dozi, alimpata demu akiwa amemgoja kwa hamu na ghamu amtimizie ahadi yake.

“Uliahidi kuwa utaninunulia pombe lakini umekuwa ukinipiga chenga. Leo ni leo na hautaondoka hapa bila kunitimizia ahadi yangu,” demu alisema.

Jamaa kwa upande wake alipuuza madai ya demu huyo na kutaka kuondoka lakini demu alimwahi na kuanza kumfokea vikali.

“Ahadi ni deni na dawa yake ni kulipa. Nataka pesa za kununua pombe. Uliniahidi lakini ukaanza kunipiga chenga. Leo hauna bahati lazima utimize ahadi,” demu alisema.

Hali iliyoonekana kuwa mzaha iligeuka na kuwa vita demu alipoweka mkono mfukoni mwa jamaa huyo akitaka kuchukua pesa kwa lazima.

Wakati demu alipozidiwa maarifa alirarua mfuko wa suruali ya polo na wateja wakajawa na hamaki na kumzaba makofi huku wakimfokea vikali.

“Kwenda kabisa mwanamke usiye na heshima wewe. Hauna haya kurarua mfuko wa suruali ya mwanamume ukitaka akupe pesa kwa lazima.

Siku hizi umeanza kuvuna usikopanda. Ukiendelea na tabia hiyo tutakuchukulia hatua na tukupige marufuku kuingia hapa na katika baa zote mjini hapa,” wateja walisema.

Wakati demu alipozidiwa na ghadhabu za wateja alichomoka mbio na kwenda kujificha chooni kabla ya kuondoka. Hata hivyo haikujulikana polo alikuwa na uhusiano gani na mwanadada huyo.

…WAZO BONZO…

 

You can share this post!

Mkasa wa Solai: KHRC yalaumu taasisi za serikali

TAHARIRI: Majaribio ya kuiba mitihani yazimwe

adminleo