Viongozi Pwani wataka 'mtu wao' ateuliwe kuongoza Bandari ya Mombasa
Na WINNIE ATIENO
BAADHI ya viongozi kutoka Pwani sasa wanataka serikali kuu kumteua Mpwani kuongoza Bandari ya Mombasa baada ya kufutwa kazi kwa Catherine Mturi-Wairi. Wanasiasa hao vilevile wanaitaka serikali kuu kueleza wazi sababu za kumfuta kazi Bi Mturi-Wairi.
“Inasikitisha kuwa serikali ilikosa kutafuta mpwani mwingine achukue hatamu na wakampa mtu ambaye hatoki eneo hili. Nitawasilisha swala hili bungeni,” mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya alisema.
Bw Baya alisema eneo la Pwani haliwezi kusherehekea madaraka sababu kampuni zilizoko eneo hilo zinaongozwa na watu kutoka bara.
“Kwani mama zetu hawawezi kuzaa watoto ambao wanaweza kuongoza kampuni hizi? Tutaongea kuhusu mpatano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga endapo maswala ya dhulma za kazi zitaangaziwa na suluhu lipatikane,” akaongeza.
Naibu gavana wa Kilifi Gideon Saburi alisema alisikitishwa baada ya Bi Mturi kusimamishwa kazi kwa muda.
“Naomba viongozi wa pwani kuchunguza sababu za kusimamishwa kazi kwa Bi Wairi na kuwaelezea Wakenya ukweli,” akasema kwenye sherehe za madaraka huko Kilifi katika uwanja wa Karisa Maitha.
Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Asha Hussein aliitaka serikali ifuate sheria katika kufuta na kuwaajiri watu kazi.
“Imekuwa kawaida kwa Mpwani kutomaliza hatamu yake kila anapochaguliwa kuwa mkurugenzi wa bandari ya Mombasa. Viongozi wa pwani ni sharti tumtetee mama yetu. Majuzi tu tulifurahia mwanamke kuchaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa bandari lakini sasa amefutwa tusinyamaze,” akasema.
Bi Wairi alisimamishwa kazi mnamo Jumatano wiki iliyopita kwa kile bodi ya bandari ilisisitiza kushindwa kukabiliana na matatizo katika bandari hiyo na uzembe wa kazi hali iliyosababisha msongamano mkubwa.
Bodi ya bandari ilitangaza kuwa ilimsimamisha kazi kwa muda Bi Wairi baada ya bandari hiyo kushindwa kuwapelekea wateja wake mizigo sababu ya msongamo.