Kimataifa

Wanafunzi wa shule za upili wanaolishana uroda barabarani waonywa

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na VALENTINE OBARA 

OSLO, NORWAY

WANAFUNZI wanaofuzu kutoka shule za upili wameonywa dhidi ya kufanya ngono katika mizunguko ya barabara.

Mamlaka ya kusimamia uchukuzi Norway iliripotiwa kusema kumekuwa na tabia ya wanafunzi kufanya ngono kwenye mizunguko ya barabara katika wiki ya mahafala ya kufuzu kutoka shule za upili.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, tabia hii hufanya madereva kukosa kuwa waangalifu barabarani na kusababisha ajali.

Nchini humo, imeripotiwa kuwa tabia zingine zinazoshuhudiwa kutoka kwa wanafunzi hao ni kukimbia madarajani wakiwa uchi wa mnyama, mbali na unywaji wa pombe kupita kiasi hadharani.

“Kila mtu anafahamu kwamba ni hatari kwa binadamu kuwa kwenye mizunguko ya barabara. Ni hatari pia mtu kukimbia uchi kwenye daraja lakini pia madereva wanaweza kushtuka ghafla na kusahau kwamba wanaendesha magari,” msimamizi wa mamlaka ya barabara za umma nchini humo, Terje Moe Gustavsen, alinukuliwa kusema kwenye vyombo vya habari.

Mbali na haya, ilisisitizwa kuwa mienendo hii ni upotovu wa maadili ya kijamii na haifai kushuhudiwa.