• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Sodo zatajwa sababu ya mimba za mapema Pwani

Sodo zatajwa sababu ya mimba za mapema Pwani

Na KAZUNGU SAMUEL

WASICHANA wengi katika eneo la Pwani hupata mimba za mapema kwa sababu ya kufanya mapenzi wakiwa na matumaini ya wavulana kuwanunulia sodo.

“Wasichana wengi hutegemea wavulana kuwapatia pesa za kununua sodo na kubadilishana hili kwa kufanya ngono. Jambo hili linasikitisha sana,” akasema kiongozi wa wa mpango wa Gift a Child, Bi Diana Chitsaka kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Bi Chitsaka, ambaye ni muuguzi katika hospitali moja katika Kaunti ya Kilifi alisema kuwa wasichana wengi hufika hospitalini wakiwa na magonjwa ya kuambukizwa baada ya kutumia vitambara wanapokosa sodo.

“Tunasikitika kwamba wasichana wengi hupata mimba ambazo hawakuzitarajia na wanalazimika kuingia maisha ambayo hawakuyategemea kamwe,” akasema Bi Chitsaka.

Tayari baadhi ya walimu wameelezea wasiwasi kuhusiana na dhiki za wasichana wakiwa shuleni wakati wakiwa na hedhi.

Vile vile aliwalaumu waendeshaji pikipiki za boda boda kuwa kiini cha mimba hizo hasa wanapowataka kimapenzi wasichana hao baada ya kuwasaidia kuwanunulia sodo.

Mmoja wa walimu Mkasi Palia, alisema kuwa wasichana wengine huamua kubakia nyumbani wakati wakiwa katika hedhi.

“Jambo hili limekuwa kero kwa ustawi wa elimu katika eneo la Pwani. Tunajua hili linatatizwa na changamoto ya umaskini ambao umeathiri jamii zetu kwa muda mrefu,” akasema Bi Palia.

“Wasichana wengi hawawezi kupata vitambaa vya hedshi na hivyo basi wanatumia matambara ambayo sio salama kiafya. Jambo hili lazima lipate suluhisho la kudumu,” akaongeza.

You can share this post!

Gavana akataza maafisa kuongea na wanahabari

Wanaharakati wapinga uchimbaji wa makaa ya mawe Lamu

adminleo