Jombi wa kunyemelea wajane kijijini aona cha mtema kuni
Na JOHN MUSYOKI
MASINGA, MACHAKOS
KALAMENI mmoja kutoka sehemu hii alikemewa vikali na wakazi kwa tabia ya kuwanyemelea wajane kijijini.
Penyenye zinasema kuwa jamaa hakuasi ukapera licha ya kufikisha umri wa kuoa na hakupenda kuchumbia mabinti mtaani.
Cha kushangaza ni kuwa jamaa alikuwa akinyemelea wajane na kuwahangaisha kwa kuvuja mali yao.
Hata hivyo, tabia yake ilikasirisha wakazi waliojua njama yake na wakapanga kumchukulia hatua.
Siku ya kioja jamaa alipokuwa kwa mjane mmoja mwendo wa saa mbili usiku baadhi wa wakazi walifika na kuanza kumfokea vikali. “Hautalala hapa leo.
Una akili timamu wewe. Hauna haya mtu mzima kama wewe kurandaranda kwa maboma ya wajane na kukesha kwao kana kwamba ni kwako.
Haujaoa na hata hauchumbii mabinti mtaani. Unafanya nini kwa wajane. Kuanzia leo tunakupa onyo la mwanzo na la mwisho. Tukikupata kwenye boma za wajane tutakuonyesha cha mtema kuni,” wakazi walisema.
Jamaa alipoambiwa atoke boma ya mjane huyo alinuna na kupuuza agizo la wakazi. Hata hivyo, juhudi zake hazikufua dafu wakazi walipomnyanyua juu na kumfurusha.
“Nenda kabisa, unataka nini hapa na sio kwako. Unakatalia hapa kwa nini. Wewe ni mtu bure kabisa. Nenda ukaoe mke wako,” wakazi walizidi kufoka. Alipomtaka mjane huyo kumtetea kama mwenyeji wake, alikataa na kumwambia aondoke.
Ilibidi jamaa kutoka shoti kuhepa ghadhabu za wakazi kwa sababu wengine walikuwa tayari wamebeba fimbo kumtwanga.
Inasemekana baadhi ya wajane walikuwa wamepanga njama na wakazi baada ya kuchoshwa na tabia ya polo ya kuwanyemelea.